Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Aziza Mangosongo amewaongoza wajumbe wa Kamati ya Lishe ngazi ya Halmashauri wakati wa kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mkataba wa lishe kwa kipindi cha robo ya pili Oktoba hadi Disemba 2023/2024.
Kupitia kikao hicho ambacho kimefanyika Februari 9, 2024 DC Mangosongo amewaelekeza watendaji wote wa Kata na Vijiji ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kuhakikisha wanasimamia kikamilifu utekelezaji wa afua za lishe kwenye maeneo yao.
Ili kukabiliana na tatizo la lishe duni na utapiamlo kwa watoto hususani wanafunzi Mkuu huyo wa Wilaya ameagiza walimu kwa kushirikiana na jamii kuhakikisha wanafunzi kwenye shule zote za msingi na sekondari wanatumia unga wenye virutubisho.
Aidha ametoa maelekezo kwa watendaji wa kata kusimamia na kufuatilia ufungwaji wa mashine zitakazozalisha unga wenye virutibisho kwenye maeneo yao na kwamba kila mmiliki wa mashine ya kuzalisha unga ahakikishe unga unaozalishwa unaongezwa virutubisho.
Vilevile ameagiza kuanzishwa kwa Klabu za Lishe kwenye kila shule ambapo pamoja na shughuli nyingine shule kupitia klabu hizo zihakikishe zinakua na bustani za matunda na mbogamboga ili chakula wanachopata wanafunzi shuleni kiwe na mchanganyiko wenye virutubisho mbalimbali.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Wilaya ya Mbinga ametoa wito kwa wanaume kwenye jamii kushiriki utekelezaji wa afua za lishe kwa kushirikiana na wake zao badala ya jukumu hili muhimu la kutokomeza lishe duni na utapiamlo kuachiwa akimama na watoto pekee.
"Utekelezaji wa afua za lishe ni jukumu letu sote kuielimisha na kuihamasisha jamii kutambua umuhimu wa lishe ili kukabiliana na udumavu, lakini wajibu wa lishe umebaki kwa wanawake na watoto tu, Ni wakati wetu sasa kuhakikisha jinsia ya kiume wanashiriki na kupata elimu ya lishe ili kuimarisha afya zetu" Amesisitiza DC Mangosongo.
Pia Mhe. Mangosongo ameagiza kuhuishwa kwa sheria ndogo za vijiji zinazowabana wazazi wenye watoto kushiriki utekelezaji wa afua za lishe pamoja na kuwapeleka kliniki kwa ajili chanjo, kufanya ufuatiliaji wa karibu na kutoa elimu pamoja na kuchukua hatua dhidi ya watoto wanaozaliwa na uzito pungufu pamoja na utapiamlo mkali
Imeandikwa na Salum Said
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
9 Februari 2024
MBINGA DISTRICT COUNCIL
Sanduku la posta: P.O. BOX 194 MBINGA-RUVUMA
Namba za simu: 2552640005
SImu ya mkononi: PS 0754533018
parua pepe: ded@mbingadc.go.tz
Copyright ©2021 Mbinga District Council. All rights Reserved. Prepared by ICT - Unit