Na Silvia Ernest,
Afisa Mwandikishaji Jimbo la Mbinga Vijijini Paschal Ndunguru amewataka waandishi wasaidizi pamoja na waendesha vifaa vya Bayometriki Jimbo la Mbinga Vijijini kuwa waadilifu na kufanya kazi kwa weledi huku wakizingatia sheria na miongozo iliyopo katika zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.
Wito huo umetolewa wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya uboreshaji wa daftari la kumudu la wapiga kura kwa Waandishi wasaidizi pamoja na Waendesha vifaa vya Bayometriki uliofanyika tarehe 9 Januari 2024.
" Haya mafunzo yamelenga kuwaongezea weledi na ufahamu kuhusu hili zoezi lililopo mbele yenu, sasa basi tuhakikishe tunatumia umahiri katika kufanikisha zoezi hili" Amebainisha
Sambamba na hilo amewataka kuzingatia muda elekezi wa kufungua vituo vya kujiandikisha ili ifikapo saa mbili asubuhi wananchi waanze kupata huduma na kupata muda wa kuendelea na majukumu yao ya kila siku.
Aidha amewataka kutunza vifaa ambavyo vitatumika wakati wote wa zoezi hilo akisisitiza kuwa Serikali imetumia fedha nyingi katika unuuzi wa vifaa , hivyo kila mmoja ana wajibu wa kutunza na kuhakikisha usalama wa vifaa unakuwepo.
Kwa upande wake Afisa kutoka Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Nicholaus Natay amewataka maafisa hao kuzingatia mafunzo yatakayotolewa ili kurahisisha na kuhakikisha utekelezaji wa zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura linakamilika bila changamoto yoyote.
Naye Afisa Uchaguzi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Andrew Mbunda ametoa rai kwa washiriki hao kuwa na nidhamu na kutoa huduma bora kwa wananchi wanaokwenda kuwahudumia na kuepuka mazoea katika utendaji kazi.
Akizungumza kwa niaba ya washiriki hao Mwandishi msaidizi ambaye pia ni mwenyekiti wa mafunzo hayo Elizabeth Banzi ameahidi kuwa watazingatia maelekezo yatakayotolewa na kufuata miongozo wakati wote wa utekelezaji.
Mafunzo haya yatafanyika kwa muda wa siku mbili kuanzia tarehe 9 hadi10 Januari 2024 na zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura Mkoa wa Ruvuma litaanza rasmi tarehe 12 hadi 18 Januari 2024.
MBINGA DISTRICT COUNCIL
Sanduku la posta: P.O. BOX 194 MBINGA-RUVUMA
Namba za simu: 2552640005
SImu ya mkononi: PS 0754533018
parua pepe: ded@mbingadc.go.tz
Copyright ©2021 Mbinga District Council. All rights Reserved. Prepared by ICT - Unit