Aliyekua Mweka Hazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Bw. Deodatus Mutalemwa pamoja na aliyekua Afisa Mapato wa Halmashauri hiyo, Bw. Elias Sanga wameagwa rasmi leo Julai 19 baada ya kupata uhamisho, katika hafla fupi iliyofanyika kwenye viwanja vya ofisi za Halmashauri vilivyopo Kiamili.
Hafla hiyo iliyoongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Ndg. Juma Mnwele na kuhudhuriwa na viongozi na watumishi wa Halmashauri hiyo waliopo Makao Makuu ya Halmashauri, Kiamili na Mkako imefanyika kufuatia watumishi hao kupata barua za kuhamishwa vituo vya kazi ambapo Bw. Mutalemwa anahamia Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Mkoani Dodoma, huku Bw. Sanga akihamia Halmashauri ya Wilaya ya Songea, ndani ya Mkoa wa Ruvuma.
Kupitia Hafla hiyo, pia viongozi hao wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga wamemkaribisha mtumishi Samwel Marwa ambaye amehamia Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga akitokea Wilaya ya Tarime, Mkoa wa Mara ambapo anakuchukua nafasi ya Bw. Mutalemwa kama Kaimu Mweka Hazina.
Akizungumza kwa niaba ya watumishi, Mkurugenzi Mtendaji, Juma Mnwele amewashukuru watumishi hao waliohama kwa utumishi na utendaji wao kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga uliochangia kwa kiasi kikubwa kutengeneza sura njema ya Halmashauri na kwamba yeye binafsi na watumishi wengine wamejifunza mambo mengi kutoka kwao ikiwemo uvumilivu, jitihada, utashi na kujituma kwao kulikochangia kufanikisha mipango mingi ya Halmashauri na kuendana na sera ya serikali.
“Compliances za sera na sheria zote sisi tumezifanya karibu asilimia 100; hili jambo lingekua gumu sana kama DT asingekua na utashi” Amesema Mkurugenzi Mnwele akifafanua zaidi kuwa kwa kipindi cha miaka mitatu Halmashauri imeweza kupeleka fedha zote za miradi, kutoa fedha za mikopo ya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu sambamba na kulipa posho za madiwani.
Vilevile kwa niaba ya watumishi wote wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Bw. Mnwele amemkaribisha Bw. Samwel Marwa ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga na kumhakikishia ushirikiano mkubwa kutoka kwake yeye binafsi, lakini pia kutoka kwa watumishi wote wa Halmashauri hiyo, huku akimpa wito wa kuendeleza na kuimarisha jitihada zaidi za ukusanyaji wa mapato.
“Tumefanya mambo mengi na mabadiliko mengi kwenye geti la Kitai kwa miaka hii mitatu, kwa sababu eneo lile karibu theluthi moja ya mapato yetu tunategemea pale ningekuomba sana utumie maarifa, muda wako na rasilimali tulizonazo kuona namna tutakavyoweza kupata suluhu ya eneo lile; kidogo bado tuna changamoto”. Amesisitiza Mkurugenzi Mnwele.
Imeandikwa na
Salum Said,
Afisa Habari, Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga
Tarehe 19, 2021 Kiamili
MBINGA DISTRICT COUNCIL
Sanduku la posta: P.O. BOX 194 MBINGA-RUVUMA
Namba za simu: 2552640005
SImu ya mkononi: PS 0754533018
parua pepe: ded@mbingadc.go.tz
Copyright ©2021 Mbinga District Council. All rights Reserved. Prepared by ICT - Unit