Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Mkoani Ruvuma wameiomba serikali kuweka mfumo rafiki utakaowezesha soko la mahindi lililopo kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula, NFRA linawafikia na kuwanufaisha wakulima wadogo, badala ya mfumo uliopo sasa ambao unawanufaisha zaidi wafanya biashara, madalali na wakulima wakubwa.
Kupitia azimio lililowasilishwa wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani robo ya nne kwa mwaka wa fedha 2020/2021 kilichofanyika leo Agosti 31 katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Kigonsera, Madiwani hao pamoja na kuipongeza serikali kufuatia uamuzi wake wa kununua mahindi kupitia NFRA, lakini pia wameeleza kutoridhishwa kwao na mfumo uliopo na mwenendo mzima wa ununuzi wa zao hilo la mahindi.
Akiwasilisha azimio hilo kwa niaba ya madiwani, Mhe. William Mbwambo ambaye ni Diwani wa Kata ya Matiri na Katibu wa Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, amesema wao kama madiwani na wawakilishi wa wananchi wanaiomba serikali kutathmini hali ya mwenendo wa soko na kuona umuhimu wa kuboresha mfumo uliopo wa ununuzi wa zao la mahindi ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya vituo vya ununuzi na kiasi cha tani zitakazonunuliwa kupitia NFRA.
Mhe. Mbwambo amesema kwa kuzingatia hali ya uzalishaji na jiografia ya Wilaya ya Mbinga kituo pekee kilichopo cha Kigonsera hakimsaidii kabisa mkulima mdogo kwani Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga ina takribani Kata nane zenye uzalishaji mkubwa wa zao la mahindi ambazo ni Mkako, Kigonsera, Amanimakolo, Namswea, Muungano, Matiri, Lukarasi na Ruanda lakini ni Kata ya Kigonsera tu ndio yenye kituo cha ununuzi wa zao hilo chini ya NFRA na ambacho kimepangiwa kununua tani 200 pekee za mahindi.
Aidha, ameongeza kuwa wakulima wengi wanashindwa kufikia soko hilo kutokana na umbali na gharama kubwa za usafirishaji kutoka kwenye maeneo ya uzalishaji hadi eneo kilipo kituo cha ununuzi, lakini pia hakuna utaratibu rasmi wa kuwatambua wakulima wadogo hali inayopelekea wakulima wengi kushindwa kuuza mahindi yao kupitia soko hilo na badala yake wameendelea kuuza mazao yao kwa bei ya chini ya wastani wa shilingi 12,000/= hadi 15,000/= kwa gunia kwenye maeneo waliyopo.
“Gharama ya kusafirisha gunia moja la mahindi kutoka kijiji cha barabara kata ya Matiri hadi Kigonsera ni shilingi 10,000, tunaiomba serikali ione uwezekano wa kusogeza vituo vya ununuzi kwenye maeneo yote yenye uzalishaji mkubwa ikiwa ni pamoja na kuainisha kiwango cha mahindi kitakachonunuliwa kutoka kwenye maeneo hayo ili kutoa fursa ya kuwafikia wakulima wengi zaidi kutoka kila eneo la uzalishaji”. Amesema Mhe. Mbwambo
Akifafanua kuhusu athari zinazoweza kujitokeza kutokana na wakulima wa zao la mahindi kuendelea kukosa soko la uhakika, Diwani Mbwambo amesema wakulima wengi watashindwa kumudu gharama kubwa za pembejeo kwa msimu ujao wa kilimo hali inayoweza kupelekea kushuka kwa uzalishaji, kuathirika kiuchumi na hatari ya kuzuka kwa baa la njaa.
Imeandikwa na
Salum Said
Afisa Habari, Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga
Agosti 31, 2021
MBINGA DISTRICT COUNCIL
Sanduku la posta: P.O. BOX 194 MBINGA-RUVUMA
Namba za simu: 2552640005
SImu ya mkononi: PS 0754533018
parua pepe: ded@mbingadc.go.tz
Copyright ©2021 Mbinga District Council. All rights Reserved. Prepared by ICT - Unit