Uwanja wa kwanza wa kisasa wa mpira wa kikapu (Basketball) Wilayani Mbinga umezinduliwa leo Aprili 30.
Hafla ya uzinduzi wa uwanja huo uliopo Shule ya Sekondari ya Wasichana Mbinga (Mbinga Girls) imefanyika shuleni hapo huku Mgeni Rasmi akiwa ni Afisa Mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Bi. Amina Kibunde aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji ambaye pia aliambatana Afisa Elimu Sekondari, Mhandisi wa Ujenzi, Afisa Taaluma, Afisa Michezo na Afisa Utamaduni wa Halmashauri hiyo.
Bi. Amina ameongeza kusema kuwa michezo mashuleni imekua na umuhimu mkubwa katika kukuza afya ya mwili na akili na kutoa wito kwa viongozi na wanafunzi wa shule hiyo kutumia vema fursa ya uwepo wa uwanja huo shuleni hapo kwa kuhakikisha wanashiriki michezo kikamilifu huku wazingatia kutunza uwanja huo ili uweze kudumu kwa muda mrefu.
Naye Bi. Rehema Rohomoja ambaye ni Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Mbinga amemshukuru Mkurugenzi Mtendaji na uongozi mzima wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kwa kuwajengea uwanja huo wa kisasa huku akiahidi matumizi sahihi na matunzo ya uwanja huo na kwamba kutokana na umuhimu wa michezo katika kuboresha afya ya mwili na akili wanatarajia kuongeza kiwango cha ufaulu shuleni hapo
Awali akisoma taarifa ya mradi wa ujenzi wa uwanja huo, Afisa Michezo Bw. Charles Maero amesema mradi huo umetekelezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga na kugharimu shilingi milioni 7, fedha zote zikiwa ni mapato ya ndani (Own Source)
Hafla ya uzinduzi wa uwanja huu imehudhuriwa pia na walimu na wanafunzi kutoka shule za sekondari za Mbinga Girls, Kigonsera, Kiamili, Mkako na Maposeni ambao pia wamepata fursa ya kushiriki midahalo na michezo mbalimbali.
Ujenzi wa uwanja huu ambao ni wa kwanza wa kisasa Wilayani Mbinga ni utekelezaji wa mkakati wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga katika kuboresha sekta ya michezo mashuleni.
Katika hatua nyingine Halmashauri imeendelea na uboreshaji wa uwanja wa michezo wa Shule ya Msingi Juhudi huku ikijiandaa kuanza ujenzi wa viwanja viwili kimoja kikiwa kwa ajili ya mpira wa miguu na kingine mpira wa kikapu Shule ya Sekondari ya Wavulana Mbinga (Mbinga Boys) iliyopo Ndongosi.
Imeandikwa na
Salum Said,
Afisa Habari, Mbinga D.C
MBINGA DISTRICT COUNCIL
Sanduku la posta: P.O. BOX 194 MBINGA-RUVUMA
Namba za simu: 2552640005
SImu ya mkononi: PS 0754533018
parua pepe: ded@mbingadc.go.tz
Copyright ©2021 Mbinga District Council. All rights Reserved. Prepared by ICT - Unit