Wawakilishi wa jumuiya za wafanyakazi kupitia Kikao cha Baraza la Wafanyakazi Wilaya ya Mbinga limeridhia na kupitisha mapendekezo ya mpango na bajeti ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kwa kipindi cha mwaka ujao wa fedha 2023/2024.
Kikao hicho chini ya Mwenyekiti wake ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Juma Haji Juma kimefanyika Kiamili Alhamisi tarehe 16 Aprili 2023 na kuhudhuriwa na viongozi na wawakilishi kutoka vyama vya wafanyakazi vya TALGWU, TUGHE na CWT, pamoja na Menejimenti ya Halmashauri hiyo.
Akiwasilisha taarifa ya mapendekezo ya mpango na bajeti ya Halmashauri kwa mwaka ujao wa fedha Kaimu Afisa Mipango wa Halmashauri Hamidu Lipweche amesema katika kipindi cha mwaka 2023/2024 Halmashauri hiyo inakisia kukusanya/kupokea na kutumia jumla shilingi Bilioni 42 kupitia vyanzo vyote vya mapato ikiwa ni pamoja na ruzuku ya serikali kuu.
Aidha amebainisha kuwa mwaka ujao wa fedha Halamashauri ya Wilaya ya Mbinga inatarajia kukusanya mapato ya ndani (own sources revenue collection) kiasi cha shilingi Bilioni 6.72 ikiwa ni ongezeko la Bilioni 2.13 sawa na 46.4% kulinganisha na bajeti ya mwaka huu 2022/2023 yenye makisio ya shilingi Bilioni 4.59
Kabla ya kufunga kikao wajumbe waliridhia kwa kauli moja kupitisha mpango na bajeti ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kwa mwaka 2023/2024 ambapo Mwenyekiti wa kikao aliwashukuru wajumbe kwa mjadala mzuri na wenye tija na hivyo ni imani ya kila mmoja kwamba maoni na michango yao itawezesha kupatikana kwa mpango unaotekelezeka.
Imeandikwa na Salum Said
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Tarehe 16 Februari, 2023
MBINGA DISTRICT COUNCIL
Sanduku la posta: P.O. BOX 194 MBINGA-RUVUMA
Namba za simu: 2552640005
SImu ya mkononi: PS 0754533018
parua pepe: ded@mbingadc.go.tz
Copyright ©2021 Mbinga District Council. All rights Reserved. Prepared by ICT - Unit