Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa amewaagiza Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano Serikalini kujituma kwa kasi, ari na weledi katika utoaji taarifa na huduma za habari kwa umma juu ya masuala mbalimbali yanayotekelezwa na serikali ikiwemo miradi ya maendeleo.
Mhe.Bashungwa ameyasema hayo Mei 24, 2021 Jijini Mbeya wakati akifungua Kikao Kazi cha Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano wa Serikali katika Ukumbi wa Mikutano uliopo Chuo cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), ambapo amesisitiza kuwa utoaji wa taarifa kwa umma ni takwa la kisheria na jamii ina haki ya kuhabarishwa huku akisema maafisa habari ndio watekelezaji wakubwa wa sheria hizo.
"Nimeguswa na Kauli Mbiu ya kikao hiki kwa mwaka huu isemayo Utoaji Taarifa kwa Umma ni Takwa la Kisheria Viongozi wa Umma na Maafisa Habari Tuwajibike, Hivyo Wizara ninayoisimamia inaendelea kufanya mageuzi makubwa katika kusimamia utoaji wa huduma za habari kwa umma, na hii ni utekelezaji wa Sheria ya Huduma ya Habari ya Mwaka 2016, na Sheria ya Haki ya Kupata Habari ya Mwaka 2016" amesisitiza Mhe. Bashungwa.
Aidha Mhe.Bashungwa ametumia nafasi hiyo kuwahakikishia Maafisa Habari kuwa Wizara yake inatambua changamoto mbalimbali zinazowakabili maafisa hao ikiwemo ukosefu na ufinyu wa bajeti, kukosa zana za kisasa na vitendea kazi muhimu kama camera, lens, computer, internet na mawasiliano, baadhi yao kutoshirikishwa kwenye vikao na ziara muhimu, pamoja na kukosa mafunzo ya mara kwa mara kulingana na mabadiliko ya teknolojia hali inayopelekea wengi wao kufanya kazi kwenye mazingira magumu.
Mhe. Waziri amewahahakishia maafisa habari hao kuwa serikali kupitia Wizara ya Habari kwa kushirikiana na Wizara nyingine hususani TAMISEMI imekusudia na kujipanga kushughulikia kikamilifu changamoto zote wanazokabiliana nazo huku akitoa wito kwa viongozi wa Wizara, Taasisi, Wakala na Mamlaka za Serkali za Mitaa kuhakisha wanatoa na kuwapa ushirikiano mzur maafisa habari hao ambao ndio washauri wakuu wa masuala ya habari kwenye maeneo yao.
Hata hivyo wakati kikao kinaendela Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Dkt. Abbasi alipokea ujumbe wa simu kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan kwenye kikao hicho ambapo akisoma ujumbe huo wa Mhe. Rais, Dkt.Abbasi amenukuu
"Naomba muendelee kuhimizana kuhusu umuhimu wa taarifa kwa Umma, yale yasiyo mazuri na yasiyo ya lazima kuwe na namna bora ya kutoa taarifa na msiache kusema mpaka wananchi waanze kulalamika ndiyo watoe taarifa"
Kikao Kazi hiki cha siku tano cha Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano wa Serikali kitakachofanyika Mei 24-28 kimehudhuriwa pia na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Dkt. Hassan Abbasi, Katibu Mkuu OR-TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe, Naibu Katibu Mkuu Habari, Dkt. Ally Possi, Naibu Waziri wa Habari Mhe. Pauline Gekul, na viongozi wengine wa Wizara na Mkoa wa Mbeya wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Juma Homera.
Imeandikwa na
Salum Said
Afisa Habari, Mbinga D.C
MBINGA DISTRICT COUNCIL
Sanduku la posta: P.O. BOX 194 MBINGA-RUVUMA
Namba za simu: 2552640005
SImu ya mkononi: PS 0754533018
parua pepe: ded@mbingadc.go.tz
Copyright ©2021 Mbinga District Council. All rights Reserved. Prepared by ICT - Unit