Leo Ijumaa Disemba 30, 2022 Benki ya NMB imekabidhi pikipiki 3 kwa maafisa Ushirika kutoka Halmashauri za Mkoa wa Ruvuma zinazolima Kahawa ili kuongeza tija katika usimamizi, ufuatiliaji na uzalishaji wa zao hilo.
Hafla ya makabidhiano ya Pikipiki hizo imefanyika Ijumaa kwenye Ofisi za NMB Mbinga Mjini ambapo Kaimu Meneja wa NMB Tawi la Mbinga Anold Mwakabage amekabidhi pikipiki 3, kadi za usajili, kofia ngumu, na viakisi mwanga (reflectors) kwa Maafisa Ushirika kutoka Halmashauri za Wilaya ya Mbinga, Mji wa Mbinga na Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa.
Akikabidhi pikipiki hizo Bw. Mwakabage amesema kufuatia kikao cha wadau wa zao la Kahawa kilichofanyika mwezi Mei mwaka huu 2022 wao kama Benki na wadau wakubwa wa zao hilo na kilimo kwa ujumla waliona kuna umuhimu wa kuwezesha vitendea kazi hasa usafiri kwenye Ofisi za Ushirika za Halmashauri hizo tatu ili kurahisisha ufuatiliaji na utoaji wa huduma za ugani kwa wakulima na vyama vya ushirika.
Aidha Afisa Uhusiano NMB Mbinga Joseph Raphael Rimoy amesema kwa kutambua umuhimu wa Ofisi za Ushirika kwenye Halmashauri na changamoto zilizopo za kijiografia kwenye maeneo ya vijijini wanakofanyia kazi wao kama Benki na wadau wametoa pikipiki hizo wakiamini zitasaidia kurahisisha wakulima wengi zaidi kufikiwa katika suala zima la upatikanaji wa huduma za ugani kutoka Ofisi za Ushirika.
"Sisi kama Benki ya NMB tukaona tutoe vitendea kazi hivi ili kuwezesha kuwafikia wakulima wengi zaidi na kwa muda mfupi ikizingatiwa jiografia ya maeneo yetu kulinganisha na rasilimali za usafiri zilizopo kwenye Halmashauri" Ameongeza Bw. Rimoy.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga mara baada ya kupokea pikipiki Afisa Ushirika Noel Ngailo ameishukuru Benki ya NMB kwa uwezeshwaji huo na kwamba wao kama watendaji wa sekta ya Kilimo na Ushirika kwenye Halmashauri wamejipanga kikamilifu kuwahudumia wakulima na vyama vya ushirika kwa urahisi, haraka na kwa ufanisi zaidi.
"Tunashukuru kwa ushirikiano huu uliopo baina ya sekta binafsi kupitia Benki ya NMB Tawi la Mbinga na Serikali kupitia Halmashauri zetu tatu na vitendea kazi hivi vitaturahisishia sana kuwatembelea wakulima, kuwasikiliza na kutatua kero zao kwa haraka zaidi " Amefafanua Bw. Ngailo
Imeandaliwa na
Salum Said, Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga
Tarehe 30 Disemba, 2022
MBINGA DISTRICT COUNCIL
Sanduku la posta: P.O. BOX 194 MBINGA-RUVUMA
Namba za simu: 2552640005
SImu ya mkononi: PS 0754533018
parua pepe: ded@mbingadc.go.tz
Copyright ©2021 Mbinga District Council. All rights Reserved. Prepared by ICT - Unit