Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Mbinga tarehe 18, 2024 imeshiriki zoezi la usafi na utunzaji wa mazingira katika Hospitali mpya ya Halmashauri iliyopo Kigonsera Wilayani Mbinga Mkoa wa Ruvuma.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Mbinga Ndg. Hajiri Methew Kapinga amewaongoza wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Jumuiya hiyo kufyeka nyasi na kupanda miti kwenye maeneo yanayozunguka hospitali ya Halmashauri ikiwa ni katika kuhitimisha Sherehe za Wiki ya Wazazi kiwilaya zilizofanyika Kata ya kigonsera, Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga.
Sambamba na kushiriki zoezi hilo la usafi na utunzaji wa mazingira, Jumuiya hiyo imetembelea miundombinu ya hospitali ambayo ujenzi wake umekamilika lakini pia imekagua maendeleo ya miundombinu mipya ambayo ujenzi wake bado unaendelea.
Akizungumza mara baada ya zoezi hilo Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Ndg. Hajiri Kapinga ameupongeza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kwa kusimamia vizuri mradi huo wa Hospitali ya Halmashauri huku akiipongeza Serikali ya chama cha mapinduzi kwa kuwasogezea karibu wananchi huduma hiyo muhimu na hivyo kusaidia kuokoa maisha ya wananchi wa Mbinga na watanzania kwa ujumla.
Naye Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Mbinga Ndg. Angelo Madundo amesema wao kama Kamati ya Utekelezaji ya Jumuiya hiyo wanampongeza na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa usimamizi mzuri wa Ilani ya Uchaguzi.
"Sisi kama Jumuiya ya Wazazi Mbinga tunaungana na wazazi wote kumpongeza Rais wetu na Mwenyekiti wa CCM Taifa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya ya kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2025 ikiwemo ujenzi wa hospitali hii ya wilaya ya Mbinga iliyojengwa kwa viwango ambayo mpaka sasa ujenzi wake umegharimu zaidi ya shilingi Bilioni 2.3" Amesema Ngd. Madundo.
Imeandikwa na Salum Said,
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali
Tarehe 18 Aprili, 2024
MBINGA DISTRICT COUNCIL
Sanduku la posta: P.O. BOX 194 MBINGA-RUVUMA
Namba za simu: 2552640005
SImu ya mkononi: PS 0754533018
parua pepe: ded@mbingadc.go.tz
Copyright ©2021 Mbinga District Council. All rights Reserved. Prepared by ICT - Unit