Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga imeanza rasmi kutoa huduma ya vipimo na chanjo ya Homa ya Ini leo Mei 6 na viongozi na watumishi wa Halmashauri hiyo wamepata fursa ya kuhudumiwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Bw. Juma Mnwele ameongoza zoezi hilo kwa kupata huduma ya vipimo na chanjo sambamba na viongozi wengine na watumishi wa Halmashauri hiyo, zoezi ambalo limefanyika kwenye Ofisi za Halmashauri zilizopo Kiamili.
Mkurugenzi Mnwele pia ametoa rai kwa watumishi wote na wananchi kwa ujumla kuchangamkia fursa hiyo adhimu ya kupata chanjo ya Homa ya Ini na kuongeza kusema serikali imefanya jitihada kubwa kuhakikisha huduma hiyo inatolewa tena kwa gharama nafuu ikilinganishwa na gharama halisi na ambazo zimekua zikitozwa kwenye maeneo mbalimba ambayo yamekua yakitoa huduma hiyo.
Naye Mganga Mkuu wa Wilaya, Dkt. Louis Chomboko ameihakikishia jamii na kuondoa hofu juu ya usalama wa chanjo hiyo ambayo inachukua muda mfupi sana kutolewa na kufafanua zaidi kuwa huduma hiyo inatolewa kwa watu wote wenye umri wa kuanzia miaka 19 na kuendelea.
Huduma ya vipimo na chanjo ya Homa ya Ini imepangwa kutolewa kwenye miji midogo yote ya Kuandaa, Mkumbi, Maguu, Kigonsera na Matiri ambapo uzinduzi rasmi utafanyika Matiri, Jumatatu Mei 10 huku Mkuu wa Wilaya ya Mbinga akitarajiwa kuwa Mgeni Rasmi kwenye uzinduzi huo.
Kesho Ijumaa Mei 7 huduma hiyo ya vipimo na chanjo ya Homa ya Ini itaendelea kutolewa kwenye Mji Mdogo wa Kigonsera ambapo pia itatolewa wakati wa Kikao cha Baraza la Madiwani kitakachofanyika kwenye Ukumbi wa Parokia ya Kigonsera na Wah. Madiwani, watumishi na wananchi watakua na fursa ya kupata huduma hiyo.
MBINGA DISTRICT COUNCIL
Sanduku la posta: P.O. BOX 194 MBINGA-RUVUMA
Namba za simu: 2552640005
SImu ya mkononi: PS 0754533018
parua pepe: ded@mbingadc.go.tz
Copyright ©2021 Mbinga District Council. All rights Reserved. Prepared by ICT - Unit