Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Mhe. Kisare Matiku Makori ameongoza kikao cha maandalizi kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wakulima Nanenane 2024 kikao ambacho kimefanyika tarehe 3 Aprili 2024 katika ukumbi wa Gereza la Kitai, Mbinga Mkoani Ruvuma.
Mkuu wa Wilaya ameongoza wajumbe kujadili na kuweka mipangao na mikakati kuelekea maadhimisho hayo yanayotarajiwa kufanyika mwezi Agosti mwaka huu 2024, kikao ambacho kimehudhuriwa na viongozi, madiwani, watendaji wa kata na vijiji, maafisa ugani na wadau wengine wakiwemo wawakilishi wa makampuni na taasisi mbalimbali za umma na binafsi.
Awali kikao hicho kilitanguliwa na ziara ya Mkuu wa Wilaya na Kamati ya Usalama ya Wilaya ambapo alitembelea na kukagua maendeleo ya vipando na ujenzi wa vibanda kwenye viwanja vya maonesho ya Nanenane vya Aziza Mangosongo vilivyopo kijiji cha Amanimakolo Wilayani Mbinga.
DC Makori ametumia fursa hiyo pia kujitambulisha mbele ya wajumbe ikiwa ni wiki chache baada ya kuaminiwa tena na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbinga akitokea Wilaya ya Moshi Mkoani Kilimanjaro ambapo katika hotuba yake ya ufunguzi ameomba kuwepo kwa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha malengo ya serikali katika wilaya yanatelezwa.
"Nawashukuruni sana kwa jinsi ambavyo tumejadili na kuzungumza. Naombeni sana tuendelee kushirikiana katika kutekeleza majukumu yetu mengine ya kiserikali" Amesisitiza DC Makori wakati wa majumuisho ya ajenda za kikao hicho.
Aidha, katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Wilaya amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kufuatilia fedha za marejesho kutoka Ofisi ya Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) ikiwa ni 3% ya mapato yanayokusanywa na TFS wilayani Mbinga kila mwaka na kuweka mkakati wa kupendezesha na kutunza mazingira ndani ya Wilaya kwa kutumia fedha hizo.
Na Salum Said, Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali.
03 Aprili 2024
MBINGA DISTRICT COUNCIL
Sanduku la posta: P.O. BOX 194 MBINGA-RUVUMA
Namba za simu: 2552640005
SImu ya mkononi: PS 0754533018
parua pepe: ded@mbingadc.go.tz
Copyright ©2021 Mbinga District Council. All rights Reserved. Prepared by ICT - Unit