Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Mhe. Aziza Mangosongo leo Jumanne Disemba 6, 2022 amekutana na kufanya mazungumzo na wadau wa kilimo kujadili hali ya upatikanaji wa pembejeo za kilimo wilayani Mbinga.
Kikao hicho kilichofanyika katika Ofisi za Mkuu wa Wilaya kimekutanisha viongozi mbalimbali wa Wilaya na Halmashauri, Maafisa Kilimo na Ushirika, wauzaji na maawakala wa pembejeo za kilimo pamoja na viongozi kutoka Chama Kikuu cha Ushirika Mbinga (MBIFACU) na Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) kutoka maeneo yote ya Wilaya ya Mbinga.
Kikao hicho kimefanyika ili kujadiliana na kupata muafaka na makubaliano ya pamoja kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazopelekea upatikanaji hafifu wa pembejeo za kilimo hususani mbolea ya ruzuku miongoni mwa wakulima wa Wilaya ya Mbinga katika kipindi hiki ambacho tayari msimu wa kilimo ukiwa tayari umeanza.
Akifungua kikao Mkuu wa Wilaya alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuipa kipaumbele sekta ya kilimo baada ya kuongeza bajeti ya Wizara na kuweka utaratibu mzuri wa ruzuku kwenye pembejeo na kwamba kupitia utaratibu huo uliowekwa na Serikali ya Awamu ya Sita uzalishaji wa mazao ya kilimo na mnyororo wa thamani kwenye mazao ya kilimo unatarajiwa kuongezeka kwa kiwango kikubwa msimu ujao wa mavuno
Kwa mujibu wa tarifa ya mapokezi ya mbolea msimu huu wa 2022/2023 iliyowasilishwa mbele ya Mkuu wa Wilaya na Maafisa Kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga na Halmashauri ya Mji wa Mbonga imeelezwa hadi jana Disemba 6 kiasi cha tani 5,061 pekee za mbolea ndizo zimepokelewa na kuuzwa kwa wakulima kwenye Halmashauri zote mbili kati ya tani 18,861 zinazohitajika sawa na asilimia 26.8% huku changamoto zikielezwa kuwa ni pamoja na uhaba wa mawakala na vituo vya kuuzia mbolea pamoja na kile kilichoelezwa kuwa hata mawakala wachache waliopo hawana mbolea ya kutosha kuweza kukidhi mahitaji ya wakulima.
Aidha kupitia kikao hicho DC Mangosongo ameunda Kamati maalum itakayokua na jukumu la kufuatilia, kutatua na kuziwasilisha moja kwa moja Wizara ya Kilimo changamoto zote zilizobainishwa kuchangia kuzorotesha hali ya upatikanaji wa mbolea ya ruzuku huku akitoa wito kwa Chama Kikuu MBIFACU kuzisimamia AMCOS zote na kuhakikisha zinawasaidia wanachama wake na wakulima waliopo kwenye maeneo yao ambayo hakuna mawakala wanapata mbolea kwa wakati.
Imeandikwa na
Salum Said
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga
6 Disemba, 2022
MBINGA DISTRICT COUNCIL
Sanduku la posta: P.O. BOX 194 MBINGA-RUVUMA
Namba za simu: 2552640005
SImu ya mkononi: PS 0754533018
parua pepe: ded@mbingadc.go.tz
Copyright ©2021 Mbinga District Council. All rights Reserved. Prepared by ICT - Unit