Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Mhe. Aziza Mangosongo ametoa wito kwa wananchi kuchangamkia fursa ya kupata chanjo ya UVIKO-19 inayotolewa bure nchini ili kukabiliana na maambukizi ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Corona (Covid-19).
Mhe. Mangosongo ametoa wito huo leo Agosti 6 wakati alipoongoza zoezi la uzinduzi rasmi wa utoaji wa chanjo ya ugonjwa wa virusi vya Corona (Uviko 19), tukio lililofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Oddo Mwisho uliopo Ofisi za Halmashauri ya Mji wa Mbinga Mkoani Ruvuma.
Akizungumza na viongozi wa Taasisi mbalimbali za Umma na binafsi, viongozi wa dini, makampuni na wadau wengine waliohudhuria hafla hiyo ya uzinduzi wa chanjo ya UVIKO-19, DC Mangosongo amesema tukio hilo ni sehemu ya kupeana taarifa za ziada kuhusu hali ya maambukizi ya Ugonjwa unaosababishwa na Virusi vya Corona nchini pamoja na kuendelea kukumbushana kuhusu hatua muhimu za kuchukua ili kuendelea kukabiliana na wimbi la tatu la UVIKO-19 Wilayani Mbinga
Mhe. Mangosongo amesema kulingana na hali ya maambukizi ya UVIKO-19 duniani na mwenendo wa ugonjwa huo nchini na katika nchi jirani ni wazi kuwa Wilaya yetu ya Mbinga, Mkoa wa Ruvuma na Taifa kwa ujumla hatupo salama na hivyo jitihada za makusudi zinahitajika ili kukabiliana na wimbi la kuenea kwa virusi hatari vya Corona na kwamba kupata chanjo ya UVIKO-19 ni hatua mojawapo na muhimu katika kukabiliana na virusi hivyo hatari..
“…hatuwezi kusema tuko salama, hivyo ni lazima juhudi za makusudi za kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huu katika Wilaya yetu ya Mbinga zichukuliwe kwa uzito unaostahili, ila iwe kwa kuleta uelewa sahihi bila kuwatisha na kuwaogopesha wananchi”. Amesema Mkuu huyo wa Wilaya.
Aidha Mhe. Mangosongo ametoa maelekezo kwa viongozi wa ngazi zote kuonesha mfano kwa wananchi kwa kuchukua hatua zote za tahadhari za kujikinga dhidi ya UVIKO-19 huku akiagiza taasisi na maeneo yote ya kutolea huduma kuweka utaratibu wa kupunguza misongamano kwenye maeneo hayo bila kuathiri shughuli za kiuchumi na kitaasisi, kusimamia upatikanaji wa vifaa kinga kama Barakoa, Maji tiririka na Sabuni, Vipukusi mikono (Sanitizer), vipima joto (Thermal scanners) na kuhakikisha vifaa hivyo vinatumika kikamilifu wakati wote.
Amesema “Halmashauri zihakikishe maeneo yote ya umma kama vile stendi za mabasi na malori, vituo vya Bajaji na Bodaboda, bustani za kupumzika, Masoko, Misikiti, Makanisa na sehemu za burudani zinakuwa na vifaa vya kunawia mikono, maji safi tiririka na sabuni na kuhakikisha vinatumika”
Ametoa wito kwa viongozi wa dini kuhakikisha waumini wote wanachukua tahadhari zote za kujikinga na UVIKO-19 wakati wa ibada ikiwemo kuvaa barakoa, kukaa umbali usiopungua mita moja baina ya mtu na mtu sambamba na kufupisha muda wa ibada huku akisitisha mikusanyiko yote Wilayani Mbinga hadi hapo ugonjwa utakapodhibitiwa.
“Nasitisha mikusanyiko yote mikubwa ya kijamii, kidini na kisiasa mpaka ugonjwa utakapodhibitiwa na kutolewa taarifa rasmi na Wizara ya Afya; Aidha, kwa mikusanyiko ya lazima wananchi watalazimika kuomba kibali kutoka kwenye mamlaka husika” Amesema DC Mangosongo.
Naye Mganga Mkuu, Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Dkt. Louis Chomboko amebainisha vituo vitakavyotoa huduma ya chanjo ya UVIKO-19 kwa Halmashauri hiyo kuwa ni Zahanati ya Mkako, Kituo cha Afya Mapera na Hospitali ya Misheni Litembo kuanzia Jumatatu Agosti 9 na kwamba kipaumbele kitatolewa kwa watumishi wa sekta ya afya, watu wenye umri wa zaidi ya miaka 50 na wale wenye magonjwa sugu.
Imeandikwa na
Salum Said,
Afisa Habari, Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga
Agosti 6, 2021
MBINGA DISTRICT COUNCIL
Sanduku la posta: P.O. BOX 194 MBINGA-RUVUMA
Namba za simu: 2552640005
SImu ya mkononi: PS 0754533018
parua pepe: ded@mbingadc.go.tz
Copyright ©2021 Mbinga District Council. All rights Reserved. Prepared by ICT - Unit