Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Juma Mnwele leo Juni 27, 2021 ameshiriki ibada ya misa takatifu na kuongoza harambee ya kuchangia ujenzi wa Kanisa la Kigango cha Kiamili, Parokia ya Kigonsera Jimbo la Mbinga.
Ibada hiyo imefanyika kwenye viwanja vya Kigango cha Kiamili na kuongozwa na Padre Silverius Mwingira ambaye amemwakilisha Paroko wa Parokia ya Kigonsera, Paroko Thadeo Kinyero.
Akizungumza kwenye Harambee hiyo ya kuchangia ujenzi wa Kanisa Mkurugenzi Mnwele, ambaye alikua Mgeni Rasmi kwenye hafla hiyo ametoa wito kwa jamii hasa waumini kuchangia kwa moyo wote na kujitolea nguvu kazi ili kuharakisha ujenzi wa kanisa hilo na kuhakikisha wanaweka suala la kuchangia ujenzi kama ajenda ya kudumu kila wanapokutana kupitia Jumuiya zao.
Aidha Bw. Mnwele amesema anatambua kuwa kukamilika kwa kanisa hilo kutarahisisha utoaji wa huduma za kiroho kwa jamii ya eneo zima la Kiamili wakiwemo watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga ambao wanaoishi na kufanya kazi makao makuu ya Halmashauri yaliyopo hapo Kiamili.
Bw. Mnwele ameongeza kuwa Kanisa hilo pia litakua tegemeo kubwa kwa wanafunzi na watumishi wa Shule za Sekondari za Kiamili, Kampala, Shule ya Sekondari ya Wasichana Mbinga (Mbinga Girls) na Shule ya Msingi Juhudi ambazo zote zipo eneo hilo la Kiamili
Akiongoza harambee hiyo Mkurugenzi Mnwele amechangia fedha tasilimu shilingi Laki Tano (Tshs.500,000/=) kama mchango wake binafsi huku akiahidi Ofisi yake kuchangia mifuko 200 ya saruji pamoja na bati 100 aina ya IT-5 (Msauzi).
Katika Harambee hiyo jumla ya fedha tasilimu shilingi 4,285,400 zimepatikana, huku ahadi zilizotolewa zikiwa ni fedha zaidi ya shilingi Laki Saba, mifuko 215 ya Saruji na bati 200.
Awali katika mahubiri yake, Padre Mwingira alisisitiza juu ya kumuamini na kumtegemea mungu katika maisha yetu ya kila siku na umuhimu wa jamii kujitoa na kumtolea mungu katika kulijenga kanisa.
Aidha Padre huyo ametoa wito kwa jamii kujitolea na kushiriki ujenzi na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na serikali akitolea mfano miradi ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya na Ofisi za Halmashauri inayojengwa hapo Kiamili
Imeandikwa na
Salum Said, Afisa Habari Mbinga D.C
Juni 27, 2021
MBINGA DISTRICT COUNCIL
Sanduku la posta: P.O. BOX 194 MBINGA-RUVUMA
Namba za simu: 2552640005
SImu ya mkononi: PS 0754533018
parua pepe: ded@mbingadc.go.tz
Copyright ©2021 Mbinga District Council. All rights Reserved. Prepared by ICT - Unit