Elimu ya unyonyeshaji imetakiwa kuwekewa mkazo na kupewa kipaumbele ikiwa ni katika jitihada za kukabiliana na hali duni ya lishe na utapiamlo mkali kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
Hayo yamejiri wakati wa kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mikataba ya lishe kilichofanyika leo Novemba 9, 2021 Kiamili Wilayani Mbinga kujadili namna wataalam wa afya na watendaji katika ngazi mbalimbali wanavyoshiriki mapambano dhidi ya utapiamlo na kuhakikisha jamii inaendelea kuwa na lishe bora Wilayani humo.
Katika kikao hicho kilichoongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Mhe. Aziza Mangosongo, na kuhudhuriwa na wataalam na Maafisa Watendaji wa Kata zote 29 za Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga imeelezwa kuwa unyonyeshaji wa watoto usiozingatia maelekezo ya wataalam unaofanywa na sehemu kubwa ya akinamama mara baada ya kujifungua ni moja ya sababu zinazochangia kuwa na hali duni ya lishe na hata kupelekea baadhi ya watoto kupata utapiamlo mkali.
Akizungumza kwenye kikao hicho Mhe. Aziza ametoa rai kwa wataalam kuweka mkazo zaidi katika kutoa elimu ya namna bora ya unyonyeshaji kwa jamii huku akikemea vikali kile kilichoelezwa tabia ya baadhi ya wanaume kunyonya maziwa ya waenza wao wanaonyonyesha na hivyo kuwakosesha watoto virutubisho muhimu, hali inayoweza kupelekea watoto kuwa na hali duni ya lishe.
Kufuatiwa kikao hicho watendaji wa Kata za Kitura, Kigonsera na Nyoni wamepongezwa kwa kufanya vizuri katika kusimamia suala la lishe kwa kipindi cha Julai hadi Septemba 2021, huku Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Mhe. Desderius Haule akipongeza utaratibu uliowekwa na Halmashauri hiyo wa kushindanisha kata na kuwatunuku zawadi Watendaji wa Kata zinazofanya vizuri.
“Kama hawa wamefanya vizuri na kushinda leo, kikao kijacho tuone kata nyingi zimefanya vizuri zaidi”. Ameongeza Mhe. Haule na kuhitimisha kuwa lishe ni suala la kimkakati kitaifa, na kwamba usimamizi thabiti wa afua za lishe kuanzia ngazi za chini (Vijiji na Kata) kutapelekea Wilaya, Mkoa na Taifa kwa ujumla kufanya vizuri na kuwa na jamii yenye lishe bora, kuongeza uzalishaji na kukuza uchumi wa nchi.
Kikao hicho kimefuatiwa na utiaji saini na uhuishwaji wa mikataba ya lishe ngazi ya Wilaya, Kata na Vijiji ambapo Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi Mtendaji, Katibu Tawala na Mganga Mkuu wa Wilaya wametia saini kwa ngazi ya Wilaya Huku Maafisa Watendaji Kata wakitia saini mikataba hiyo kwa upande wa Kata na Vijiji.
Imeandikwa na
Salum Said,
Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga
Tarehe 9 Novemba, 2021
MBINGA DISTRICT COUNCIL
Sanduku la posta: P.O. BOX 194 MBINGA-RUVUMA
Namba za simu: 2552640005
SImu ya mkononi: PS 0754533018
parua pepe: ded@mbingadc.go.tz
Copyright ©2021 Mbinga District Council. All rights Reserved. Prepared by ICT - Unit