Mtoto Baraka Nicolaus Mbunda mwenye umri wa miaka 12 na mwenye mahitaji maalum kutokana na ulemavu wa viungo alionao baada ya kuzaliwa bila miguu na mikono, hatimaye amewezeshwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kwa kupatiwa vifaa saidizi.
Baraka ambaye ni mwanafunzi wa darasa la pili shule ya msingi Huruma amekabidhiwa vifaa hivyo Januari 16, 2024 na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Mhe. Desderius Haule wakati alipomtembelea shuleni hapo kujionea hali halisi ya changamoto zinazomkabili.
Mwenyekiti Haule amemkabidhi mtoto Baraka vifaa ambavyo ni kiti-mwendo au kiti cha magurudumu (wheelchair) pamoja na kiti maalum kinachosaidia mtu mwenye mahitaji maalum wakati wa kupata haja kubwa na ndogo ikiwa ni hatua za awali zilizochukuliwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga katika kumpunguzia adha na changamoto mtoto huyo kutokana na hali ya ulemavu aliyonayo.
Mara baada ya kukabidhi vifaa hivyo Mhe. Haule amebainisha kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga itaendelea kufuatilia kwa ukaribu maendeleo ya mtoto Baraka na kwamba kuna jitihada mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa katika kuwafikia watoto wengi zaidi wenye mahitaji maalum na kushughulikia changamoto zinazowakabili ikiwemo ujenzi wa shule maalum ya watu wenye ulemavu inayojengwa Kata ya Maguu.
“Halmashauri itafanya kila kitakachowezekana kuhakikisha mtoto Baraka anasoma na kufikia ndoto zake kama alivyoeleza mwenyewe hapa kwamba anataka asome hadi awe Daktari” Amesisitiza Mwenyekiti Haule.
Katika hatua nyingine Mwenyekiti huyo wa Halmashauri ametoa wito kwa wazazi na walezi pamoja na jamii kwa ujumla kutowaficha watoto wenye ulemavu na kwamba wanatakiwa kuthaminiwa na kupewa haki kama watoto wengine.
Akizungumzia hali ya taaluma ya Baraka shuleni Mkuu wa Shule ya Msingi Huruma Sr. Augusta Mlelwa amesema tangu alipoanza masomo yake shuleni hapo Baraka amekua na maendeleo mazuri sana kitaaluma kwani muhula wa kwanza akiwa darasa la kwanza alishika nafasi ya kwanza darasani huku muhula wa pili akishika nafasi ya pili kati ya wanafunzi 59 waliofanya mtihani.
Mapema mwezi Disemba 2023 Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Juma Haji Juma mara baada ya kupata taarifa za mtoto Baraka alimulekeza Afisa Ustawi wa Jamii Bw. Filbert Mahay kumtembelea mtoto huyo nyumbani kwao kijiji cha Ugogo kilichopo Kata ya Mikalanga ambapo baada ya kujionea hali halisi ikabainishwa hatua ya haraka ni kumuwezesha vifaa hivyo saidizi.
Imeandikwa na Salum Said
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga
MBINGA DISTRICT COUNCIL
Sanduku la posta: P.O. BOX 194 MBINGA-RUVUMA
Namba za simu: 2552640005
SImu ya mkononi: PS 0754533018
parua pepe: ded@mbingadc.go.tz
Copyright ©2021 Mbinga District Council. All rights Reserved. Prepared by ICT - Unit