Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Bi. Aziza Mangosongo ametoa wito kwa jumuiya ya wafanyabiashara, wadau na wananchi wote kulitazama eneo la Kiamili, mahali zilipo ofisi na Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kama kitovu kipya cha fursa za kiuchumi na uwekezaji kwa Wilaya ya Mbinga na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla.
Hayo yamejiri wakati wa kikao cha Baraza la Biashara kilichofanyika Jumatano Novemba 23 na kuhudhuriwa na wafanyabiashara na wadau wengine kutoka kwenye makundi mbalimbali ya uwakilishi wa wafanyabiashara na wajasiriamali wilayani Mbinga.
Katika kikao hicho pamoja na mambo mengine zimejadiliwa fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo eneo la Kiamili zilipo Ofisi na Makao Makuu ya Halmashauri ikiwa ni pamoja na uwepo wa fursa kemkem za uwekezaji kwenye sekta ya elimu, michezo, masoko na maduka makubwa, fursa za kibiashara kwenye maeneo ya wazi yaliyotengwa, hoteli na nyumba za kulala wageni na kwamba tayari eneo hilo limepimwa na kutengwa viwanja kwa ajili ya huduma mbalimbali za kijamii kama makazi, makazi na biashara, uwekezaji na kutengwa kwa maeneo ya kuzikia.
Kwa kipindi cha takribani mwaka mmoja tu kutoka Oktoba 2021 hadi Novemba 2022 tangu Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kuhamishia Makao yake Makuu eneo la Kiamili kutoka Mbinga mjini eneo hilo lililopo kilometa 30 kutoka Mbinga mjini na kilometa 67 kutoka Manispaa ya Songea limekua na kasi kubwa ya ukuaji wa kiuchumi na kijamii ambapo tayari huduma zote muhimu za kijamii kama umeme, maji, barabara zinapatikana ndani ya eneo hilo sambamba na uwepo wa hospitali ya Halmashauri inayotarajiwa kuanza kutoka huduma hivi karibuni.
Imetolewa na
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga
23 Novemba, 2022
MBINGA DISTRICT COUNCIL
Sanduku la posta: P.O. BOX 194 MBINGA-RUVUMA
Namba za simu: 2552640005
SImu ya mkononi: PS 0754533018
parua pepe: ded@mbingadc.go.tz
Copyright ©2021 Mbinga District Council. All rights Reserved. Prepared by ICT - Unit