Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga imepongezwa kwa usimamizi mzuri wa miradi mara baada ya Kamati ya Siasa Wilaya ya Mbinga kutembelea na kufanya ukaguzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa ndani ya Halmashauri hiyo Ijumaa Machi 18, 2022.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wilayani Mbinga Beda Hyera, kwa niaba ya wajumbe wa Kamati wa Siasa amesema wao kama chama wameridhishwa sana na ubora wa miradi yote iliyotembelewa na Kamati hiyo na kwamba wanapongeza uongozi wa Halmashauri kwa kusimamia vema miradi hiyo.
Naye Bi. Kurusumu Mhagama ambaye ni Mjumbe wa UWT Mkoa wa Ruvuma amewashukuru na kuwapongeza wananchi wote wanaoendelea kuunga mkono jitihada za serikali kwa kujitolea nguvukazi katika ujenzi wa miundombinu kwenye maeneo yao na kutoa rai kwa serikali kuhakikisha shughuli ndogo zilizosalia hususani kwenye ujenzi wa Kituo cha Afya Mkumbi zinakamilishwa haraka ili wananchi waanze kupata huduma.
Jumla ya miradi minne imetembelewa na wajumbe wa Kamati ya Siasa Wilaya ya Mbinga ambayo ni Ujenzi wa Kituo cha Afya Mkumbi, Vyumba vitatu vya madarasa Shule ya Sekondari Mkumbi yaliyojengwa kupitia mradi wa TCRP (UVIKO-19), ujenzi wa Hospitali ya Wilaya eneo la Kiamili Kata ya Kigonsera na ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari ya mfano inayojengwa kupitia program ya SEQUIP kata ya Amanimakolo.
Ziara hii ya wajumbe wa Kamati ya Siasa imefanyika ikiwa ni ukaguzi wa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ngazi ya Wilaya kwa kipindi cha 2020/2025.
Na Salum Said, Mbinga
Tarehe 18 Machi, 2022
MBINGA DISTRICT COUNCIL
Sanduku la posta: P.O. BOX 194 MBINGA-RUVUMA
Namba za simu: 2552640005
SImu ya mkononi: PS 0754533018
parua pepe: ded@mbingadc.go.tz
Copyright ©2021 Mbinga District Council. All rights Reserved. Prepared by ICT - Unit