Kiongozi wa Mbio Maalum za Mwenge wa Uhuru mwaka huu 2021 Lt. Josephine Mwampashe ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kwa usimamizi na utekelezaji mzuri wa miradi yote ya maendeleo iliyotembelewa na Mwenge huo.
Luteni Mwampashe ametoa pongezi hizo leo Septemba 4, 2021 baada ya kuridhishwa na hali ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambayo amesema ni matokeo ya usimamizi mzuri kufuatia Mwenge wa Uhuru uliowasili mapema leo hii Wilayani Mbinga kukagua, kutembelea, kuweka jiwe la msingi na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga
Mradi wa kwanza ambao umekaguliwa na Kiongozi wa Mbio Maalum za Mwenge wa Uhuru mwaka huu ni Klabu wa Wapinga Rushwa katika Shule ya Sekondari ya wasichana Mbinga (Mbinga Girls) Klabu ambayo awali ilizinduliwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2018 yenye jumla ya wanachama 16 ambapo amepongeza uendelevu wa mradi huo.
Miradi mingine ni Jengo la Uthibiti Ubora wa Elimu lenye thamani ya Tshs. Milioni 181.8 ambalo limezinduliwa, Ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri iliyowekwa jiwe la Msingi, mradi ambao hadi kukamilika kwake utagharimu Tshs. Milioni 500 katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wake unaotarajiwa kukamilika Disemba mwaka huu 2021.
Katika hatua nyingine Kiongozi wa Mbio Maalum za Mwenge Lt. Josephine Mwampashe amekagua Kikundi cha Vijana cha Chipukizi kinachojishughulisha na ufyatuaji wa tofali za zege ambacho pia ni moja kati ya vikundi vilivyowezeshwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kupitia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri hiyo kwa kupatiwa mkopo wa Tshs. Milioni 22 kwa mwaka wa fedha 2020/2021
Mwenge wa Uhuru umekimbizwa Wilayani Mbinga baada ya kupokelewa kijiji cha Mkako ukitokea Wilaya ya Namtumbo na unatarajiwa kukabidhiwa kesho Septemba 5 Wilayani Nyasa katika Kijiji cha Mkalole ambapo ukiwa Wilayani Mbinga umetembelea jumla ya miradi nane yenye thamani ya Tshs. Bilioni 3.14 kutoka Halmashauri zote mbili za Wilaya na Mji wa Mbinga.
Miradi mingine minne iliyopitiwa na Mwenge wa Uhuru kutoka Halmashauri ya Mji wa Mbinga ni Mradi wa Maji, Redio Hekima FM, Nyumba ya Mkurugenzi wa Mji pamoja na mradi wa Barabara ya Lami inayotekelezwa na Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini TARURA Wilaya ya Mbinga.
Imeandikwa na
Salum Said,
Afisa Habari, Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga
4 Septemba 2021
MBINGA DISTRICT COUNCIL
Sanduku la posta: P.O. BOX 194 MBINGA-RUVUMA
Namba za simu: 2552640005
SImu ya mkononi: PS 0754533018
parua pepe: ded@mbingadc.go.tz
Copyright ©2021 Mbinga District Council. All rights Reserved. Prepared by ICT - Unit