Na Silvia Ernest
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Joseph Kashushura amewataka watendaji wa Vijiji kuhakikisha fedha zote zinazokusanywa katika maeneo yao zinapelekwa benki ili kuondoa mianya ya upotevu wa fedha unaosababishwa na matumizi ya fedha mbichi.
Mkurugenzi Kashushura ametoa agizo hilo katika kikao chake na Watendaji wa Vijiji kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano uliopo katika Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga tarehe 4 Julai 2024.
“Fedha zote zinazokusanywa zipelekwe benki ili zitumike kwa utaratibu sio unakusanya tu fedha unaanza kutumia bila kufuata utaratibu hii haipo sawa na yeyote atakae bainika atachukuliwa hatua ” Amesisitiza Mkurugenzi Kashushura
Sambamba na hilo amewataka kusimamia ukusanyaji wa mapato pamoja na kutambua vyanzo vyote vya mapato vilivyopo katika maeneo yao ili fedha hiyo itumike katika ktekeleza miradi ya maendeleo.
Aidha amewataka watendaji hao kuwa na utaratibu wa kusikiliza kero za wananchi na kusisitiza kuwa hataki kusikia wananchi wanapoteza muda wao kuja Makao makuu ya Halmashauri kuwasilisha kero zao ambazo zingetatuliwa katika ngazi ya Kijiji.
Vilevile Mkurugenzi Kashushura amewataka viongozi hao kuhakikisha wanasimamia miradi ya maendeleo katika maeneo yao ikiwa ni moja ya majukumu yao katika kuhakikisha utekelezaji unaofanywa na Serikali unaleta tija kwa wananchi.
Pia ameendelea kuwasisitiza viongozi hao kusoma taarifa za mapato na matumizi ya Kijiji ili kuleta uwazi na uelewa kwa wananchi wa makusanyo na matumizi wa fedha katika kutekeleza shughuli za Serikali.
MBINGA DISTRICT COUNCIL
Sanduku la posta: P.O. BOX 194 MBINGA-RUVUMA
Namba za simu: 2552640005
SImu ya mkononi: PS 0754533018
parua pepe: ded@mbingadc.go.tz
Copyright ©2021 Mbinga District Council. All rights Reserved. Prepared by ICT - Unit