Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga imepanga kujenga shule maalumu itakayohudumia na kutoa elimu kwa watoto wenye ulemavu na wanaohitaji uangalizi maalumu ikiwa ni jitihada za Halmashauri hiyo kusaidia kundi hilo muhimu.
Akizungumza kwenye kikao cha kujadilia changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu kilichofanyika leo Aprili 16, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Juma Mnwele amesema shule hiyo inayokusudia kuhudumia watoto wote wenye mahitaji maalumu itajengwa Kata ya Maguu.
Mkurugenzi Mnwele amesema Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga imepanga kutekeleza ujenzi wa shule hiyo utakaogharimu shilingi Milioni 250 kwa awamu na kwamba kuanzia Julai Mosi mwaka huu Halmashauri hiyo imekusudia kutumia shilingi Milioni 100 ambazo tayari zimetengwa kwenye mpango wa bajeti wa mwaka 2021/2022 zikazotumika kujenga madarasa mawili, vyoo na bweni.
Bw. Mnwele ameongeza kwa kusema katika kuhakikisha azma ya kujenga shule hiyo inatimia, tayari Ofisi yake imepanga ziara ya wajumbe wa Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango ya Halmashauri ambao watatembelea Kata ya Maguu na kukagua eneo la ujenzi wa shule hiyo, ziara inayotarajiwa kufanyika Jumatatu Aprili 19.
Naye Bi. Happy Mpete ambaye ni Afisa Elimu Maalumu amesema serikali imekua ikichukua jitihada mbalimbali kusaidia jamii ya watoto wenye ulemavu kwa kuajiri walimu wenye elimu maalumu pamoja na kujenga miundombinu rafiki kwa wenye mahitaji maalumu pamoja na kuweka vitengo maalumu kwa watoto wenye ulemavu hususani wasioona, wenye ukiziwi watoto wenye ulemavu wa akili.
Bi. Mpete amesema Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga ina walimu 23 wenye elimu maalumu, huku akizitaja shule zenye vitengo vyenye watoto wenye mahitaji maalumu kuwa Shule ya Msingia Litumbandyosi ambayo inahudumia watoto wenye ukiziwi na Shule ya Msingia Halale inayohudumia watoto wenye ulemavu wa akili.
Kikao cha Tathimini kujadili changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu kilichofanyika leo Ijumaa Aprili 16 katika ukumbi wa Sifina uliopo Kigonsera kimeandaliwa na kuratibiwa na Chama cha Watu Wenye Ulemavu (CHAWATA) na Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemamavu (SHIVYAWATA) Wilayani Mbinga kwa kushirikiana na shirika la The Foundation of Civil Society, FCS.
Awali wakizungumza kwenye kikao hicho, mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Mhe. Cosmas Nshenye, viongozi wa CHAWATA na SHIVYAWATA Wilayani Mbinga waliomba serikali kufanya utambuzi wa watu wenye ulemavu kuanzia ngazi ya chini utakaokuza na kuongeza takwimu za uandikishaji wa shule kwa watoto wenye ulemavu sambamba na kuweka miundombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu kwenye maeneo yote ya kutolea huduma.
Akichangia kuhusu suala la uandikishaji wa watoto waliofikia umri wa kuanza shule, Mkuu huyo wa Wilaya ya Mbinga amesema suala hilo linahitaji ushirikiano na uwajibikaji wa pamoja baina ya familia, jamii na serikali na kwamba wajibu wa kwanza unaanza ngazi ya famili.
“Familia ambayo ina mtoto mwenye ulemavu aliyefikia umri wa kwenda shule ila hajaandikishwa kisheria familia hiyo inatakiwa kuwajibishwa na kushughulikiwa”. Amesema Mhe. Nshenye.
Shule hii kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalumu inayotarajiwa kujengwa Kata ya Maguu itakua shule ya tatu maalumu kwa Halmshauri ya Wilaya ya Mbinga; Shule mbili za awali zikiwa ni Shule ya Sekondari ya Wasichana Mbinga Girls iliyopo Kiamili Kata ya Kigonsera, na Shule ya Sekondari ya Wavulana Mbinga Boys iliyopo Ndongosi Kata ya Namswea; zote zikijengwa na kuendeshwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kupitia mapato yake ya fedha za ndani yaani Own Source Revenue Collections.
Imeandikwa na:
Salum Said
Afisa Habari
HALMASHAURI YA WILAYA YA MBINGA. Aprili 16, 2021
MBINGA DISTRICT COUNCIL
Sanduku la posta: P.O. BOX 194 MBINGA-RUVUMA
Namba za simu: 2552640005
SImu ya mkononi: PS 0754533018
parua pepe: ded@mbingadc.go.tz
Copyright ©2021 Mbinga District Council. All rights Reserved. Prepared by ICT - Unit