Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga imeendelea kufanya vizuri katika utekelezaji wa mkataba wa lishe kwa kuwa na 128.22% ya utekelezaji wa viashiria vya lishe ikishika nafasi ya kwanza kati ya Halmashauri 8 za mkoa wa Ruvuma kwa kipindi cha robo ya tatu kuanzia Januari hadi Machi 2021/ 2022.
Akiwasilisha taarifa ya hali ya lishe wilayani Mbinga wakati wa kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mkataba na mapitio ya viashiria vya lishe vinavyofanyiwa kazi ngazi ya Halmashauri, Kata na Vijiji kilichofanyika Kiamili Jumatatu Juni 20, 2022 Afisa Lishe wa Halshauri ya Wilaya ya Mbinga Bi. Janeth Bandari amesema Halmashauri hiyo imeongoza katika utekelezaji wa viashiria vyote na kushika nafasi ya kwanza katika matokeo ya jumla ya utekelezaji wa afua za lishe huku Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo ikishika nafasi ya Pili.
Bi. Bandari amefafanua baadhi ya vigezo na viashiria vya lishe ambavyo Halmashauri hiyo imefanya vizuri kuwa ni pamoja na kufanyika kwa vikao vya lishe ngazi ya wilaya kwa kila robo mwaka, idadi ya watoto wenye utapiamlo mkali waliopatiwa matibabu, utoaji wa elimu ya ulishaji watoto wadogo na wachanga kwa wazazi na walezi, pamoja na uwepo wa taarifa za hali ya lishe zilizohuishwa kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
Ameongeza kuwa utekelezaji wa mkataba wa lishe katika robo ya 3 umefanyika kwa kuwapatia wazazi na walezi elimu ya ulishaji wa watoto wadogo na wachanga 9,991 kati ya 8,517 waliokusudiwa sawa na 117%, upimaji wa hali ya lishe kwa watoto 41,575 huku mtoto mmoja akibainika kuwa na utapiamlo mkali sawa na 0.002%, jumla ya wajawazito 8,202 walipatiwa nyongeza ya vidonge vya kuongeza damu, utoaji wa elimu ya lishe katika shule za msingi na sekondari, uzinduzi wa klabu za lishe shule ya sekondari mkako pamoja na utoaji wa mafunzo kwa waratibu 58 walioko kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Lishe ya Wilaya ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Bi. Aziza Mangosongo amepongeza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kwa kuendelea kufanya vizuri katika usimamizi na uboreshaji wa hali za lishe za wananchi wa Mbinga na kutoa wito kwa Afisa Lishe na Mganga Mkuu wa Wilaya kuhakikisha wanafanya ufuatiliaji wa maendeleo ya wale wote wanaobainika kuwa na hali mbaya ya lishe huku akisisitiza ulaji wa vyakula vyenye virutubisho vyote muhimu sambamba na kila mmoja kutenga muda wa kufanya mazoezi.
Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga imekua na mwendelezo wa kufanya vizuri katika utekelezaji wa mkataba wa lishe hadi ngazi ya chini ya kata na kijiji kwa mujibu wa afua na viashiria vyote vya lishe vilivyowekwa ambapo kwa kipindi cha robo zote tatu mfululizo kuanzia Julai hadi Machi 2021/2022 Halmashauri hiyo imeongoza kwa kushika nafasi ya kwanza kati ya Halmashauri zote 8 za Mkoa wa Ruvuma.
Na Salum Said, Juni 20, 2022 Kiamili-Mbinga.
MBINGA DISTRICT COUNCIL
Sanduku la posta: P.O. BOX 194 MBINGA-RUVUMA
Namba za simu: 2552640005
SImu ya mkononi: PS 0754533018
parua pepe: ded@mbingadc.go.tz
Copyright ©2021 Mbinga District Council. All rights Reserved. Prepared by ICT - Unit