Kamati ya Siasa Wilaya ya Mbinga imepongeza jitihada zinazofanywa na Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga katika kuweka mazingira rafiki na salama ya kujisomea na kujifunzia kwa watoto wenye mahitaji maalum wilayani humo.
Hayo yamejiri Alhamisi Disemba 22, kufuatia ziara ya Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Mbinga ilipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Shule ya Msingi ya Bweni inayojengwa Kijiji cha Maguu, mahsusi kwa ajili ya watoto wenye ulemavu na wenye mahitaji maalum.
Akizungumza mara baada ya kukagua ujenzi wa mradi huo Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Mbinga Ndg. Augustino Joseph Mdaka amempongeza Mkurugenzi Mtendaji na Timu yake ya Wataalamu na Madiwani kwa kuamua kujenga Shule hiyo maalum kabisa kwa watoto wenye ulemavu.
Ndugu Mdaka amesema mradi huo wa Shule utakapokamilika utasaidia kuweka mazingira rafiki na salama ya kujisomea na kujifunzia kwa watoto wenye ulemavu ambao wamekua wakikabiliwa na changamoto mbalimbali wanapopata elimu kwenye shule za mchanganyiko na hivyo kuathiri maendeleo yao ya kitaaluma.
"Sisi kama Kamati ya Siasa tumeona jitihada kubwa zilizofanyika hapa na tunakupongeza Mkurugenzi na timu yako kwa kuamua kutekeleza mradi wa namna hii ambao utakapokamilika utawasaidia vijana wetu wenye mahitaji maalum kuwa na mazingira mazuri ya kupata elimu na hatimaye kuweza kujitegemea kwenye maisha yao ya mbeleni". Ameongeza Mwenyekiti huyo.
Shule hiyo ya Msingi ya watoto wenye mahitaji maalum inajengwa kijiji cha Maguu kilichopo Kata ya Maguu, Tarafa ya Hagati, Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kwa kutumia fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri ambapo hadi sasa kiasi cha shilingi Milioni 150 zimepelekwa shuleni hapo na tayari vyumba 4 vya madarasa, Ofisi 2 za walimu na matundu 11 ya vyoo yameshajengwa huku ujenzi wa bweni la wanafunzi 80 ukiwa unaendelea
MBINGA DISTRICT COUNCIL
Sanduku la posta: P.O. BOX 194 MBINGA-RUVUMA
Namba za simu: 2552640005
SImu ya mkononi: PS 0754533018
parua pepe: ded@mbingadc.go.tz
Copyright ©2021 Mbinga District Council. All rights Reserved. Prepared by ICT - Unit