Wananchi wa Wilaya ya Mbinga wameaswa kuzingatia ushauri na maelekezo ya wataalamu wa afya ya lishe juu ya ulaji unaofaa wa makundi mbalimbali ya chakula ili kukabiliana na uwepo wa wimbi kubwa la jamii yenye udumavu na utapiamlo mkali katika maeneo yao.
Wito huo umetolewa Alhamisi tarehe 10 Novemba 2022 na Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Bi. Aziza Mangosongo wakati akizungumza na wananchi waliojitokeza kwenye maadhimisho ya Siku ya Afya ya Lishe kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga yaliyofanyika Kata ya Ngima, Tarafa ya Mkumbi.
Mhe. Mangosomo amesema wananchi wa Wilaya ya Mbinga na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla ni wazalishaji wakubwa wa mazao ya chakula, huku mengi yakisafirishwa kwenda mikoa mbalimbali na nje ya nchi na kwamba ni aibu kubwa kwa wananchi hawa ambao Taifa linawategemea kwa usalama wa chakula kuendelea kukumbwa na tatizo la ukosefu wa lishe bora.
Mkuu huyo wa wilaya amesema ili kukabiliana na tatizo la lishe duni, udumavu na utapiamlo mkali jamii inatakiwa kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa afya ya lishe juu ya ulaji bora wa chakula unaozingatia mlingano, mpangilio na uwiano sahihi wa makundi mbalimbali ya vyakula ili kuupatia mwili virutubisho vyote vinavyohitajika kwa ajili ya lishe na afya bora.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Wilaya amempongeza Mkurugenzi Mtendaji Juma Haji Juma, na uongozi mzima wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kwa utekelezaji mzuri wa mkataba wa lishe kwa vitendo na kwamba anatambua namna ambavyo Halmashauri hiyo imekua ikitenga fedha za kutosha kila kwaka kwa ajili ya utekelezaji wa afua za lishe sambamba na usimamizi mzuri wa utekelezaji wa mikataba ya lishe kwenye vijiji na kata.
“Natambua Halmashauri hii inaongoza na ni kinara katika utengaji wa fedha na utekelezaji wa afua za lishe; nakuomba Mkurugenzi uendelee kuweka jitihada zaidi za kusimamia suala la lishe kuwa ajenda ya kudumu kwenye vikao vyote kuanzia ngazi ya kijiji, kata hadi huku wilayani” Amesema DC Mangosongo
Awali akiwasilisha taarifa ya lishe mbele ya Mkuu wa Wilaya; Bi. Janeth Bandari ambaye ni Afisa Lishe wa Halmashauri amesema Halmashauri hiyo imeendelea kutekeleza muongozo wa kutenga shilingi 1,000/ kwa mtoto na kwamba mwaka huu wa fedha 2022/2023 jumla ya shilingi Milioni 92.7 zimetengwa kwa watoto 42,543 kwa ajili ya kutekeleza afua mbalimbali za lishe, sawa na wastani wa shilingi 2,179/ kwa kila mtoto.
Amesema hadi sasa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga imefanikisha kutoa elimu ya ulishaji watoto wadogo na wachanga, kutoa vigonge vya madini chuma kwa akina mama wajawazito, matone ya nyongeza ya Vitamin A kwa watoto umri chini ya miaka 5 ambapo watoto wote 36,166 waliolengwa kwa kipindi cha kuanzia Julai hadi Agosti wamefikiwa.
Maadhimisho haya ya Siku ya Afya ya Lishe yaliambatana na zoezi la upimaji wa hali ya lishe kwa jamii kwa kuangalia uwiano wa urefu na uzito, maonesho ya aina na makundi mbalimbali ya vyakula pamoja na mafunzo na elimu ya namna ya kuandaa uji wa lishe, unyweshaji uji na unyonyeshaji watoto wadogo na wachanga, na kwamba tayari kata 23 kati ya 29 za Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga zimeshafanya maadhimisho haya, sawa na asilimia 79.
Imeandaliwa na
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga
Tarehe 10 Novemba, 2022
MBINGA DISTRICT COUNCIL
Sanduku la posta: P.O. BOX 194 MBINGA-RUVUMA
Namba za simu: 2552640005
SImu ya mkononi: PS 0754533018
parua pepe: ded@mbingadc.go.tz
Copyright ©2021 Mbinga District Council. All rights Reserved. Prepared by ICT - Unit