Mafunzo ya elimu ya lishe na ufuatiliaji wa shughuli za lishe kwenye kata na vijiji imeanza kutolewa leo Mei 20, ikiwa ni mkakati Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga katika kukabiliana na tatizo la udumavu na utapia mlo kwa jamii.
Elimu hiyo imetolewa na wawezeshaji kutoka Kamati ya Lishe ya Wilaya ambao walioongozwa na Afisa Lishe, Bi. Janeth Bandari kwa wahudumu wa afya vijijini (WAVI) kutoka kwenye vijiji vyote vya kata za Mkumbi, Kipololo, Ukata, Linda na Kitumbalomo ikiwa ni utekelezaji wa mkataba wa lishe ngazi ya Kata na Vijiji.
Pamoja na elimu hiyo iliyoambatana na ulaji na uzingatiaji wa mlo kamili unaojumuisha makundi matano ya vyakula, pia wahudumu hao ambao ndio watekelezaji wakuu wa shughuli za lishe kwenye vijiji na vitongoji wameaswa kuzingatia maelekezo wanayopewa ili kuibua na kupata takwimu sahihi za watoto walio chini ya umri wa miaka mitano wenye hali nzuri ya lishe, walio na udumavu na utapia mlo na kwa wakati.
Mafunzo hayo pia yameambatana na elimu ya utunzaji wa mazingira na matumizi ya choo bora kwa kaya na jamii iliyotolewa na Bw. Abbas Rasoul, ambaye ni Afisa Afya wa Wilaya ili kuepukana na milipuko ya magonjwa ya kuambukiza na yanayoenezwa kutokana na mazingira machafu.
Imeandikwa na
Salum Said,
Afisa Habari, Mbinga D.C
MBINGA DISTRICT COUNCIL
Sanduku la posta: P.O. BOX 194 MBINGA-RUVUMA
Namba za simu: 2552640005
SImu ya mkononi: PS 0754533018
parua pepe: ded@mbingadc.go.tz
Copyright ©2021 Mbinga District Council. All rights Reserved. Prepared by ICT - Unit