Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga wamekutana kupitia mkutano wa kawaida wa Baraza la Madiwani kujadili utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Halmashauri hiyo kwa kipindi cha robo ya pili ya mwaka kuanzia Oktoba hadi Disemba 2022/2023.
Mkutano wa Baraza la hilo la Madiwani umefanyika Jumatano Februari 15, 2023 katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Kigonsera na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali ngazi ya Wilaya wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Mhe. Aziza Mangosongo.
Akitoa salamu za serikali mbele ya wajumbe wa baraza na wageni waalikwa Mkuu wa Wilaya ya Mbinga pamoja na mambo mengine amewataka viongozi kusimamia kikamilifu miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye maeneo yao na kutoa wito kwa kila mmoja katika jamii kusimamia maadili hususani maelezi bora kwa watoto.
Baraza hilo la Madiwani chini ya mwenyekiti wake ambaye pia ni mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Desderius Haule na Katibu wa Baraza ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Juma Haji Juma limepitia na kujadili taarifa na utendaji kazi wa Kamati za Kudumu za Halmashauri kwa kipindi cha robo ya pili ya mwaka huu wa fedha ulioanza Julai 2022.
Aidha, Taasisi za serikali ambazo ni pamoja na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) na Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi na Mazingira Vijijini (RUWASA) zimeweza kuwasilisha taarifa za utendaji kazi wao kwa kipindi cha robo ya pili ambapo wajumbe wameweza kupata nafasi ya kuchangia mawasilisho hayo.
Mkutano huo wa Baraza la Madiwani umekutanisha pia Madiwani wa Kata na wale wa Viti Maalum, Menejimenti ya Halmashauri, wataalamu wakiwemo watendaji wa Kata zote 29 za Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, viongozi wa dini, wawakilishi wa makundi maalum wakiwemo viongozi wa Chama cha Watu Wenye Ulemavu Wilaya ya Mbinga (CHAWATA) na wageni wengine waalikwa.
Imeandikwa na
Salum Said
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
MBINGA DISTRICT COUNCIL
Sanduku la posta: P.O. BOX 194 MBINGA-RUVUMA
Namba za simu: 2552640005
SImu ya mkononi: PS 0754533018
parua pepe: ded@mbingadc.go.tz
Copyright ©2021 Mbinga District Council. All rights Reserved. Prepared by ICT - Unit