Wilaya ya Nyasa imekua mwenyeji wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Mkoani Ruvuma kwa mwaka huu 2023 ambapo sherehe za kilele cha maadhimisho hayo zimefanyika Jumatano tarehe 8 Machi 2023 katika viwanja vya bandari mjini Mbambay na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi kutoka Wilaya na Halmashauri zote za Mkoa wa Ruvuma.
Akihutubia mbele ya wananchi Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thoma ambaye alikua Mgeni Rasmi wakati wa maadhimisho hayo ametoa wito wa kuwepo kwa mshikamano na ushirikiano miongoni mwa wanawake huku akikemea vikali vitendo vya ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto vinavyoendelea kutokea na kuripotiwa kila mara.
Kanali Thomas ameitaka jamii kupiga vita vitendo vya ubakaji, ulawiti na ushoga vinavyoelezwa kusababishwa kwa kiasi kikubwa na mmomonyoko wa maadili miongoni mwa jamii na kuongeza kuwa vitendo hivyo vinahatarisha usalama na ni kinyume kabisa na mila, utamaduni na desturi za kiafrika na kutoa wito kwa jamii kuendelea kushirikiana na Serikali katika kupiga vita vitendo hivyo.
Kabla ya kupokea maandamano ya wanawake kutoka taasisi, idara za umma na binafsi, kampuni na sekta rasmi na zisizo rasmi sherehe hizo zilizofana kwa ukubwa wake na kuambatana na shamrashamra za kila aina zilitanguliwa na matukio ya Mgeni Rasmi kukagua shughuli za wajasiriamali kwenye vibanda vya maonesho, kukagua vikundi vya ngoma za asili zilizojitokeza kutumbuiza.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa amezindua Jukwaa la Uwezeshwaji Wanawake Kiuchumi Mkoa wa Ruvuma ambapo amesema jukwaa hilo ni kwa ajili ya kila mwanamke bila kujali itikadi zao za kisiasa.
MBINGA DISTRICT COUNCIL
Sanduku la posta: P.O. BOX 194 MBINGA-RUVUMA
Namba za simu: 2552640005
SImu ya mkononi: PS 0754533018
parua pepe: ded@mbingadc.go.tz
Copyright ©2021 Mbinga District Council. All rights Reserved. Prepared by ICT - Unit