Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amewataka wananchi na jamii ya Mkoa huo kuchukulia suala la utunzaji wa vyanzo vya maji kama sehemu ya utamaduni, desturi na utaratibu wa kawaida kwenye maisha yao ya kila siku.
RC Thomas ametoa wito huo leo Jumatatu tarehe 13 Machi, 2023 wakati wa hafla ya utoaji wa zawadi na motisha kwa wananchi na jumuiya zilizofanya vizuri katika kuhifadhi na kutunza vyanzo vya maji kwenye maeneo mbalimbali ya Wilaya za Mbinga na Nyasa Mkoani Ruvuma.
Katika hotuba yake kama Mgeni Rasmi kwenye hafla hiyo ambayo imefanyika kwenye ofisi za Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Mbinga mjini leo Jumatatu tarehe 13 Machi 2023 Mkuu huyo wa Mkoa amesema utunzaji wa vyanzo vya maji ni jukumu la kila mmoja huku akisisitiza suala la upandaji wa miti na utunzaji wa miti hiyo ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.
"Utunzaji wa vyanzo vya maji ni jukumu la kila mmoja wetu ikiwa ni pamoja na upandaji wa miti rafiki na kuhakikisha miti hiyo inalindwa na kutunzwa". Amesema RC Thomas.
Akitoa maelezo ya utangulizi kuhusiana na hafla hiyo ya kuwatunuku zawadi wananchi waliofanya vizuri katika utunzaji wa vyanzo vya maji Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Nyasa Mhandisi Elice Mnally amesema suala la zawadi ni utu lakini kutunza vyanzo vya maji ni wajibu wa kila mmoja na ni suala la maisha yetu, ustaarabu wetu na afya zetu kwa ujumla.
"Jitihada hizi tunazoziweka ni kwa sababu mkoa wa Ruvuma una vyanzo vingi vya maji na tuna wajibu wa kuhakikisha tunavitunza vyanzo hivi ili viweze kutusaidia kwenye maendeleo yetu ya kiuchumi lakini hata vizazi vinavyofuata." Amesisitiza Mhandisi Mnally.
Halfa hii imeandaliwa na Wizara ya Maji kupitia Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Nyasa na ni kufuatia ziara ya Waziri wa Maji Mhe. Juma Aweso mwaka 2022 alipotembelea miradi na vyanzo vya maji kwenye maeneo mbalimbali wilayani Mbinga na Nyasa na kuridhishwa na hali ya uhifadhi na utunzaji wa vyanzo hivyo ambapo alitoa ahadi ya kuchangia mifuko 150 ya saruji kwa ajili ya kuendeleza miradi ya maji ya jamii kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Halmashauri ya Mji Mbinga na Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa.
Imeandikwa na Salum Said
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga
MBINGA DISTRICT COUNCIL
Sanduku la posta: P.O. BOX 194 MBINGA-RUVUMA
Namba za simu: 2552640005
SImu ya mkononi: PS 0754533018
parua pepe: ded@mbingadc.go.tz
Copyright ©2021 Mbinga District Council. All rights Reserved. Prepared by ICT - Unit