Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Mbinga Alhamisi ya tarehe 2 Februari, 2023 imekutana na wadau mbalimbali wa makaa ya mawe kujadili changamoto na uwepo wa mazingira hatarishi na mianya ya rushwa katika mfumo wa ukusanyaji wa mapato yanayotokana na ushuru wa makaa ya mawe kwenye kizuizi cha kukusanyia ushuru huo cha Kitai.
Warsha hiyo imefanyika katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari Kigonsera, Mgeni Rasmi akiwa Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Bi. Aziza Mangosongo na kukutanisha wadau wa madini ya makaa ya mawe kutoka sekta za umma na binafsi wakijumuisha Menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango ya Halmashauri, Kamati ya Usalama ya Wilaya, Maafisa Tarafa na Watendaji wote wa Kata na Vijiji.
Katika hotuba yake ya ufunguzi Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Bi. Aziza Mangosongo, ambaye alikua Mgeni Rasmi katika warsha hiyo pamoja na mambo mengine amesisitiza suala la uadilifu na uaminifu kwa watumishi wote wanaohusika na usimamizi na ukusanyaji wa mapato ya makaa ya mawe na mapato mengine ya serikali na kutoa wito kwa watu woye na mamlala zinazohusika kuendelea kuweka mikakati ya kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato.
Awali katika maelezo ya utangulizi kuhusiana na warsha hiyo Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Mbinga Frederick Msae amesema tukio hilo linafuatia zoezi uchambuzi wa mfumo wa ukusanyaji wa mapato yanayotokana na makaa ya mawe lilioendeshwa na ofisi yake kwa kipindi cha miezi michache iliyopita ambapo ufuatiliaji ulifanyika kuanzia eneo la mauzo ya makaa (sales points) kwa makampuni yote ya makaa ya mawe hadi eneo la ukaguzi na kukusanyia ushuru (check point) la Kitai.
Akibainisha zaidi juu ya kilichofanyika wakati wa ufuatiliaji wa mfumo wa mapato hayo yanayotokana na ushuru wa makaa ya mawe, Afisa wa TAKUKURU Blandina Hamisi ameeleza kwamba uchambuzi huo ulijikita katika maeneo kadhaa ambayo ni uzingatiaji wa Sheria ndogo za Halmashauri katika ukusanyaji wa ushuru wa makaa ya mawe na uwezekano wa kuwepo kwa mianya ya rushwa kwenye ukusanyaji wa ushuru huo.
Vilevile Ofisi hiyo ya TAKUKURU katika ufuatiliaji wake iliangalia changamoto na viashiria vinavyoweza kusababisha wakusanya mapato kwenye kizuizi cha Kitai kujiingiza kwenye vitendo na mazingira hatarishi na kupelekea upotevu wa mapato ambapo wajumbe waliweza kupitia na kujadili changamoto hizo, kuweka mikakati ya pamoja na hatimaye kupitisha maazimio kwa ajili ya utekelezaji.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga ameishukuru Ofisi ya TAKUKURU kwa kubainisha changamoto kwenye ukusanyaji wa ushuru na mapato yatokanayo na makaa ya mawe na tayari Ofisi yake imeanza kuchukua jitihada mbalimbali ikiwemo kufungwa kwa kamera za CCTV na kuwekwa kwa mifumo ya umeme wa jua (solar system) na Tanesco kwenye kizuizi cha mapato cha Kitai na kuongeza kuwa ofisi yake ina mkakati wa kuweka kizuizi cha kisasa kitakachokua kinatumia kadi maalumu za kieletroniki kuruhusu gari za makaa ya mawe kupita (an electronic gate pass system).
Imeandikwa na Salum Said
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Tarehe 2 Februari, 2023
MBINGA DISTRICT COUNCIL
Sanduku la posta: P.O. BOX 194 MBINGA-RUVUMA
Namba za simu: 2552640005
SImu ya mkononi: PS 0754533018
parua pepe: ded@mbingadc.go.tz
Copyright ©2021 Mbinga District Council. All rights Reserved. Prepared by ICT - Unit