Na Silvia Ernest
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Mhe.Desderius Haule amebainisha kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga itaendelea kutenga fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya ukamilishaji na utekelezaji wa miradi mipya itayokwenda kuleta tija kwa wananchi.
Haule amebainisha hayo tarehe 13 Mei 2024 akijibu swali la Diwani wa Viti maalum Kata ya Kihangimahuka Mhe. Leonora Mwinuka katika mkutano wa baraza la madiwani kujadili taarifa za robo ya tatu kuanzia mwezi Januari hadi Machi 2024 lililouliza Je Halmashauri ina mkakati gani wa kukamilisha miradi viporo.
Haule ameeleza kuwa pamoja na shughuli nyingine utekelezaji wa miradi ya maendeleo ni kipaumbele cha Halmashauri katika kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Kwa upande wake Katibu wa Baraza hilo Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Joseph Rwiza ametoa rai kwa madiwani kushirikiana na wataalam wa Halmashauri katika kukusanya mapato ili fedha hizo zitumike katika kutekeleza miradi ya maendeleo.
Aidha amebainisha kuwa pamoja na vyanzo vya mapato vilivyopo,Halmashauri inaendelea kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kuongeza mapato pamoja na kuondokana na utegemezi wa fedha kutoka Serikali Kuu pekee.
Akitoa salamu za Serikali, Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Mhe. Kisare Makori amempongeza Mkurugenzi Mtendaji kwa kusimamia ukusanyaji wa mapato na kuvuka lengo la makisio ya mapato ya ndani kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Akichangia mada katika Mkutano huo Diwani wa Kata ya Matiri Mhe. William Mbwambo ametoa rai kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudhibiti UKIMWI kuona namna bora ya kuwafikia wanawake wengi zaidi wakati wa zoezi la uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi.
MBINGA DISTRICT COUNCIL
Sanduku la posta: P.O. BOX 194 MBINGA-RUVUMA
Namba za simu: 2552640005
SImu ya mkononi: PS 0754533018
parua pepe: ded@mbingadc.go.tz
Copyright ©2021 Mbinga District Council. All rights Reserved. Prepared by ICT - Unit