Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Mhe. Aziza Mangosongo amewataka wananchi wilayani humo kuwa na desturi ya kupima afya zao mara kwa mara na kuchukua hatua za kujikinga dhidi ya maambukizi ya Virusi vya UKIMWI ili kuunga mkono jitihada mbalimbali zinazochukuliwa na serikali katika kupambana na maambukizi ya virusi hivyo hatari duniani.
Akihutubia wananchi wakati wa maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani ambayo kwa Wilaya ya Mbinga yamefanyika Kata ya Mpepai Mhe. Mangosongo amesema jamii ikihamasika kwa wingi katika suala la upimaji wa Virusi vya UKIMWI (VVU) na kila mmoja akachukua hatua mara baada ya kutambua hali ya afya yake itasaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti kasi ya maambukizi ya virusi hivyo.
Mhe. Mangosongo ameongeza kuwa upimaji wa VVU ni jambo la hiyari lakini lenye umuhimu mkubwa na limekua likisaidia hata wale wanaobainika kuambukizwa VVU kuanzishiwa mara moja matumizi ya dawa za kufubaza makali ya virusi hivyo na kutoa wito kwa jamii kuweka UKIMWI na magonjwa mengine ya zinaa kuwa ajenda ya kudumu kwenye vikao, mikutano na mikusanyiko yote kuanzia ngazi ya vijiji na kata
Aidha Mkuu huyo wa Wilaya ameongeza kuwa serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa afya imejipanga kuendelea kutoa elimu ya kinga dhidi ya VVU, elimu ya lishe na jinsi ya kuishi na VVU kwa waliombukizwa sambamba na utoaji wa elimu ya UKIMWI mahala pa kazi.
Awali akitoa taarifa kwa mgeni rasmi Bw. Andrew Kapinga, kwa niaba ya Mratibu wa Huduma za UKIMWI Kinga (DACC) Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga amesema hali ya maambukizi kwa Wilayani Mbinga kwa sasa ni asilimia 4 (4%) na kwamba jitihada mbalimbali zimekua zikichukuliwa katika mapambano dhidi ya VVU ikiwemo uhamasishaji wa tohara kwa wanaume, upimaji wa mara kwa mara na kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto
Bw. Kapinga amefafanua kuwa sababu zinazochangia ongezeko la maambukizi ya VVU kwa Wilaya ya Mbinga kuwa ni pamoja na kushamiri kwa ngono zembe, kurithi wajane na wagane, ulevi uliopindukia, umasikini miongoni mwa jamii na imani za kishirikina.
Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani hufanyika tarehe Desemba Mosi ya kila mwaka, mwaka huu yakibebwa na kauli mbiu isemayo “Zingatia Usawa, Tokomeza UKIMWI, Tokomeza Magonjwa ya Mlipuko” ambapo kwa Wilaya ya Mbinga maadhimisho hayo yamefanyika Kata ya Mpepai, Halmashauri ya Mji wa Mbinga.
Imeandikwa na
Salum Said, Mbinga
1 Desemba 2021
MBINGA DISTRICT COUNCIL
Sanduku la posta: P.O. BOX 194 MBINGA-RUVUMA
Namba za simu: 2552640005
SImu ya mkononi: PS 0754533018
parua pepe: ded@mbingadc.go.tz
Copyright ©2021 Mbinga District Council. All rights Reserved. Prepared by ICT - Unit