Viongozi na Wataalamu kutoka Wilaya ya Ileje iliyopo Mkoani Songwe leo Mei 12, 2023 wamefanya ziara kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga ambapo wametembelea maeneo mbalimbali na kujionea namna ukusanyaji wa mapato unavyofanyika kupitia shughuli za uchimbaji wa makaa ya mawe.
Timu hiyo ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Ileje Bi. Farida Mgomi imejumuisha pia Menejimenti ya Halmashauri, Kamati ya Fedha, Katibu wa Mbunge Jimbo la Ileje pamoja na viongozi wengine awali iliwasili mapema Ofisi za Halmashauri Kiamili na kupokelewa na mwenyeji wao ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri Juma Haji Juma kabla ya kuelekea kwenye mgodi wa makaa ya mawe wa Kampuni ya Jitegemee Holdings uliopo Kijiji cha Ntunduwaro, Kata ya Ruanda.
Mara baada ya kujionea namna shughuli za uchimbaji wa madini hayo unavyofanyika kwenye eneo la mgodi, timu hiyo iliyoambata na wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kutoka Idara na Vitengo vinavyohusika na usimamizi wa shughuli za ukusanyaji wa mapato imepitia na kupata maelezo kwenye eneo la kuchakata na kuuzia makaa ya mawe (sales point) la Kamapuni ya Jitegemee lililopo Paradiso.
Aidha ziara hiyo imehitimishwa kwa Timu ya Viongozi na Wataalamu kutoka Ileje ziara kutembelea kituo cha ukaguzi na ukusanyaji wa mapato cha Kitai ambapo wameweza kupata maelezo ya kina juu ya aina na namna Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga inavyosimamia makusanyo ya ushuru, tozo na mapato mbalimbali yanayotokana na makaa ya mawe.
Mara baada ya kuhitimisha ziara hiyo Mkuu wa Wilaya ya Ileje Mhe. Farida Mgomi kwa niaba ya Timu yake ameushukuru uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kwa ushirikiano mkubwa walioupata na kwamba kupitia ziara hii wamejifunza mengi ambayo wao kama viongozi na Wataalamu wataenda kuyafanyia kazi na hatimaye kuhakikisha Halmashauri na Wilaya ya Ileje inajiimarisha na kufanya vizuri kwenye ukusanyaji wa ushuru na mapato kupitia sekta ya makaa ya mawe kama ilivyo sasa kwa Halamashauri ya Wilaya ya Mbinga.
Imeandaliwa na Salum Said
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga
Tarehe 12 Mei, 2023
MBINGA DISTRICT COUNCIL
Sanduku la posta: P.O. BOX 194 MBINGA-RUVUMA
Namba za simu: 2552640005
SImu ya mkononi: PS 0754533018
parua pepe: ded@mbingadc.go.tz
Copyright ©2021 Mbinga District Council. All rights Reserved. Prepared by ICT - Unit