Na Silvia Ernest,
Wafugaji wa kuku Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga wamekumbushwa kuwachanja kuku ili kuwakinga na magonjwa mbalimbali pamoja na kupunguza gharama za matibabu pindi kuku wanapougua.
Wito umetolewa tarehe 21 Oktoba na Afisa Mifugo wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Bw. Haruna Masige alipozungumza katika kipindi cha radio MBINGA YETU kinachorushwa na Radio Hekima.
Amesema"kuanzia siku ya kwanza kifaranga anapototolewa kinatakiwa kipate chanjo, katika umri huu wa siku moja kifaranga huwa kinashambuliwa na ugonjwa unaitwa Mahepe"
Ameendelea kueleza kuwa katika siku ya 7 kuku anatakiwa apate chanjo ya ugonjwa wa Gumboro ambayo itarudiwa tena siku ya 21.
Siku ya 14 kuku anatakiwa apate chanjo ya ugonjwa wa Mdondo maarufu kama Kideri ambayo itarudiwa tena siku ya 30, kuku akiwa na umri wa miezi 2 hupewa chanjo ya ndui.
Pamoja na hayo Masige amewakumbusha wafugaji kuzingatia usafi katika banda la kufugia kuku na mazingira yake pamoja na usafi wa vyombo vya kulishia ili kudhibiti kuenea kwa magonjwa.
Kwa elimu na taarifa mbalimbali usikose kuwasikiliza wataalam kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kupitia Radio Hekima kila jumamosi kuanzia saa sita hadi saa saba mchana.
MBINGA DISTRICT COUNCIL
Sanduku la posta: P.O. BOX 194 MBINGA-RUVUMA
Namba za simu: 2552640005
SImu ya mkononi: PS 0754533018
parua pepe: ded@mbingadc.go.tz
Copyright ©2021 Mbinga District Council. All rights Reserved. Prepared by ICT - Unit