Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Joseph Rwiza amewataka waganga wafawidhi wa vituo vya kutolea huduma za afya kutekeleza majukumu yao ya kuwahudumia wananchi sambamba na kusimamia ukusanyaji wa mapato katika maeneo yao.
Rwiza ametoa agizo hilo tarehe 26 Machi 2024 katika kikao chake na timu ya uendeshaji wa huduma za afya pamoja na waganga wafawidhi wa vituo vya kutolea huduma za afya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga.
"Mwenendo wa ukusanyaji wa mapato hauridhishi kuna vituo ambavyo vina alama nyekundu hapa hakikisheni mnatimiza wajibu wenu na nyie ambao mnafanya vizuri endelezeni ari hiyo tukikutana tena nataka nione mabadiliko" Amesema
Aidha amewataka viongozi hao kuhakikisha wanaimarisha ulinzi na usalama pamoja na kuzingatia usafi wa mazingira katika maeneo yao akisisitiza kuwa mazingira safi ni moja wapo ya tiba kwa wagonjwa wanaokwenda kupata huduma katika vituo hivyo.
Kwa upande mwingine ameitaka timu ya uendeshaji wa huduma za afya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kusimamia na kufanya ufuatiliaji katika vituo vya kutolea huduma za afya ili kuimarisha utoaji wa huduma bora za afya kwa wananchi.
Kwa kipekee Mkurugenzi Rwiza ametoa pongezi kwa Zahanati ya Kigonsera kwa kusimamia vizuri ukusanyaji wa mapato yatokanayo na huduma ya bima ya CHF, amewataka washiriki wa kikao wengine kuiga mfano huo katika maeneo yao.
Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga George Mhina ameeleza kuwa katika mwaka wa fedha 2024/2025 Halmashauri imetenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa vishikwambi ambavyo vitatumika katika kukusanya mapato kwa kutumia mfumo wa kieletroniki wa GoT-HoMIS.
Ameeleza kuwa hatua hii itasaidia kuondoa udanganyifu na mianya ya upotevu wa fedha katika vituo hivyo.
Imeandikwa na Silvia Ernest
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
MBINGA DISTRICT COUNCIL
Sanduku la posta: P.O. BOX 194 MBINGA-RUVUMA
Namba za simu: 2552640005
SImu ya mkononi: PS 0754533018
parua pepe: ded@mbingadc.go.tz
Copyright ©2021 Mbinga District Council. All rights Reserved. Prepared by ICT - Unit