Wananchi wa Wilaya ya Mbinga wametakiwa kuchangamkia fursa mbalimbali zitokanazo na mianzi na bidhaa nyingine za misitu mara baada ya programu maalumu ya kuongeza mnyororo wa thamani mazao ya misitu kutekelezwa wilayani humo.
Hayo yamejiri baada ya Mkuu wa Wilaya yaMbinga na viongozi wengine wa Wilaya hiyo leo machi 29, 2021 kutembelea kikundi cha TUMEAMUA kilichopo Kata ya Ukata, Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga ambacho kinajishughulisha na ususi na uzalishaji wa bidhaa zitokanazo na mianzi.
Akizungumza na wanachama wa kikundi hicho Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Mhe. Cosmas Nshenye ambaye pia aliambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, ametoa rai kwa kikundi hicho kuongeza aina na ubora wa bidhaa wanazotengeneza jambo litakalosaidia kukuza wigo wa soko na kuongeza thamani ya bidaa hizo.
Mhe. Nshenye ameongeza kwa kusema ni vema kwa kikundi hicho pamoja na vikundi vingine vinavyojishughulisha na ususi Wilayani Mbinga kubadilisha mtazamo wao na kuchukulia shughuli hiyo kama shughuli mojawapo na muhimu ya kiuchumi
Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya waliombatana na Mkuu wa Wilaya katika ziara hiyo wametoa wito kwa kikundi hicho kufikiria kuzalisha bidhaa nyingi zaidina tofautitofauti kama vitanda, viti, makochi, stiki za mishikaki, miko, vijiko na bidhaa nyingine za jikoni zitokanazo na mianzi badala ya bidhaa pekee zinazotengenezwa na kikundi kwa sasa ambazo ni ungo, makapu, majamanda, na mikoba.
Pia kamati hiyo imeshauri juu ya umuhimu wa kikundi kuwa na mchanganyiko wa wanachama hasa vijana na wanawake ili kuwa na muendelezo na kurithisha fani hiyo kizazi kijacho sambamba na kuruhusu na kukaribisha watu wenye fani tofauti kama mafundi seremala jambo litakalowezesha kuzalisha bidhaa za aina tiofauti na zenye ubora zaidi.
Akizungumzia juu ya ziara hiyo ya viongozi wa Wilaya kutembelea miradi inayofadhiliwa na programu ya FORVAC, Bw. Marcel Mtunda ambaye ni mratibu wa FORVAC kanda ya Ruvuma amesema lengo la ziara hiyo ni kushirikisha Serikali ya Wilaya kufahamu shughuli zinazofanywa na mradi na kutoa fursa kwa viongozi hao wa wilaya kujua maendeleo ya mradi kwa kila hatua inayoendelea
Bw. Mtunda ameongeza kuwa kupitia ziara hiyo viongozi wa Wilaya wameweza kutoa ushauri kwa watekelezaji wa mradi pamoja na wananchi juu ya nini kifanyike katika kuongeza thamani ya mnyororo wa mazao ya misitu, jambo litakalopelekea uendelevu wa shughuli za mradi mara muda wa utekelezaji wa mradi utakapofika kikomo
Kikundi cha TUMEAMUA ni kati ya vikundi 20 vinavyofadhiliwa na Programu ya Kuongeza Mnyororo wa Thamani Mazao ya Misitu FORVAC Wilayani Mbinga mradi unaofadhiliwa na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Serikali ya Finland ambavyo pamoja na ususi, vikundi vingine vinajishughulisha na ufugaji wa nyuki na biashara ya uyoga.
Imeandaliwa na:
Salum Said
Afisa Habari
Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga
MBINGA DISTRICT COUNCIL
Sanduku la posta: P.O. BOX 194 MBINGA-RUVUMA
Namba za simu: 2552640005
SImu ya mkononi: PS 0754533018
parua pepe: ded@mbingadc.go.tz
Copyright ©2021 Mbinga District Council. All rights Reserved. Prepared by ICT - Unit