Wananchi Wilayani Mbinga wameaswa kuzingatia ukweli, uwazi na kujiepusha na uonevu na ukandamizaji dhidi ya watu wasio na hatia huku wakitakiwa kufuata taratibu zilizopo wakati wa kuwasilisha malalamiko yao kwa viongozi.
Hayo yamebainishwa leo Aprili 8, na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmshauri ya Wilaya ya Mbinga, Bw. Juma Mnwele aliyeambatana na Wakuu wote wa Idara na Vitengo wa Halmashauri hiyo wakati alipofanya ziara ya kutembelea Kijiji cha Kilindi kilichopo Kata ya Matiri na kuzungumza na wananchi kupitia mkutano wa hadhara uliofanyika Kijijini hapo.
Ziara hiyo ya Viongozi wa Wilaya imefanyika kufuatia maagizo aliyoyatoa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Bi. Christina Mndeme kwa viongozi hao wa Halmashauri kufuatilia ukweli na undani wa kero na malalamiko yaliyowasilishwa Ofisini kwake kupitia barua iliyoandikwa na baadhi ya wanaoelezwa kuwa wananchi wa Kijiji cha Kilindi, wakilalamikia Viongozi wa Kijiji hicho na Kata ya Matiri kwa ubadhirifu wa mali za umma sambamba na viongozi hao kujenga uhasama na chuki baina yao na baina ya wananchi.
Awali akifungua mjadala wa kupokea, kupitia na kutatua kero na malamiko mbalimbali kutoka kwa wananchi, Bw. Mnwele hiyo amesema wamekua wakipokea barua nyingi na zenye malalamiko mengi kutoka kijijini hapo na hivyo aliwataka wananchi kueleza kero na malalamiko yao kwa uwazi na kueleza kwa ukweli na kuepuka kuonea na kukandamiza viongozi ndani ya kata na watu wasio na hatia yoyote.
Baadhi ya wananchi waliozungumza kwenye mkutano huo wamesema hawaitambui barua hiyo iliyowasilishwa Mkoani wakieleza kusikitishwa kwao na jambo hilo, na kufafanua zaidi kuwa hakuna kikao wala mkutano waliokaa na kupitisha azimio la kuwasilisha barua ya malalamiko Ofisini kwa Mkuu wa Mkoa ikiwemo pia kukana kujadili na kupitisha malalamiko yaliyopo kwenye barua hiyo.
Naye Diwani wa Kata ya Matiri Mhe. William Mbwambo amewataka wananchi kuacha ushabiki na uchochezi huku akisema barua hiyo imeandikwa na watu wachache ambao wamekua na tabia ya kupandikiza chuki kwa wananchi dhidi ya viongozi wa Kijiji na Kata hali inayopelekea kuzua taharuki na mvurugano kijijini hapo na kuongeza kuwa hata yeye binafsi amekua akiambiwa mambo mengi na watu hao ambayo hayana ukweli wowote.
Barua hiyo ya tarehe 3 Machi, 2021 imeelezwa kuandikwa na watu watano (5) waliojiorodhesha kwenye barua ambao ni Leo Komba, John Nchimbi, Kastrory Komba, Shaneli Kapusanga Komba na Elias Komba; wanne kati yao wakitokomea na kushindwa kuonekana kwenye mkutano huo huku mmoja (Elias Komba) akishangaa na kupinga vikali kushiriki kuandika barua hiyo na kusema siku ambayo barua inaelezwa kuandikwa alikua safarini.
Viongozi wa Halmsahauri ya Wilaya ya Mbinga mara kwa mara wamekua wakifanya ziara ya kutembelea vijiji na kata kwa kusudio la kukutana na kuzungumza na wananchi kupitia mikutano ya hadhara ili kusikiliza kero na malalamiko, kuona msingi wa malalamiko hayo na hatimaye kuyapatia ufumbuzi ili kuendana na misingi ya utawala bora katika kuhudumia wananchi.
Imeandikwa na:
Salum Said
Afisa Habari
HALMASHAURI YA WILAYA YA MBINGA. Aprili 8, 2021
MBINGA DISTRICT COUNCIL
Sanduku la posta: P.O. BOX 194 MBINGA-RUVUMA
Namba za simu: 2552640005
SImu ya mkononi: PS 0754533018
parua pepe: ded@mbingadc.go.tz
Copyright ©2021 Mbinga District Council. All rights Reserved. Prepared by ICT - Unit