Watanzania wameaswa kuongeza hamasa na mwamko wa unywaji wa kahawa ili kuboresha afya zao sambamba na kuimarisha soko la ndani la zao hilo na hivyo kukuza uchumi wa wakulima na nchi wa ujumla.
Hayo yameelezwa leo Oktoba Mosi, 2021 na Bi. Mwanaidi Mang’uro ambaye ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbinga wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kahawa Duniani ambayo kwa Mkoa wa Ruvuma yamefanyika Kata ya Maguu Wilayani Mbinga na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa zao hilo kutoka Wilaya na Halmashauri zote za Mkoa wa Ruvuma.
Katika hotuba yake Bi. Mang’uro ambaye amemuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kama Mgeni Rasmi kwenye maadhimisho hayo amesema pamoja na kuwa na uzalishaji mkubwa wa kahawa nzuri na yenye ubora Mkoani Ruvuma lakini bado kukosa utamaduni na utaratibu wa kunywa kahawa miongoni mwa wakulima, wadau na watanzania wengi ni moja ya changamoto zinazoirudisha nyuma sekta ya Kahawa nchini.
Aidha amesema kahawa ni zao la kiuchumi na tegemezi kwa Mkoa na nchi, hivyo utamaduni na desturi ya unywaji wa kahawa utaimarisha sana soko la ndani na kupunguza utegemezi kwenye soko la kimataifa kwani bei inapoyumba katika soko la dunia huathiri moja kwa moja pato na uchumi wa mkulima na Serikali kwa ujumla
Katibu Twala huyo ameongeza kuwa tafiti za kisayansi zinaonesha kuna faida nyingi za kimwili na kiafya za unywaji wa kahawa ikiwemo kuburudisha na kuchangamsha mtumiaji, kundoa sumu za vyakula mwilini lakini pia ikielezwa kuwa kahawa ni chanzo kikubwa cha madini ya Potassium, Phosphorus, Magnesium, Calcium na Sodium na hivyo kuchangia katika kuimarisha mifupa na ukuaji wa mwili.
“Kuna dhana ilisambaa miongoni mwa watanzania kuwa unywaji wa kahawa unasababisha maradhi ya moyo, presha, kisukari na kupelekea mtumiaji kukosa usingizi”. Amefafanua Mgeni Rasmi huyo huku akiwataka watanzania kupuuzia dhana na imani hizo potofu
Vilevile Bi. Mang’uro amewataka wakulima wa kahawa kwenye maeneo yote ya Mkoa wa Ruvuma kuzingatia kanuni bora za uzalishaji wa kahawa na kusisitiza matumizi ya mitambo ya kisasa ya kuchakata kahawa (CPU) ili kukidhi ubora na kuongeza thamani na bei ya zao hilo sokoni huku akionya kuepuka kuchakata kahawa majumbani.
“Lengo la Serikali ni kuona kahawa yote inayozalishwa inaandaliwa kwenye mitambo ya kisasa ya kuchakata kahawa ili kukidhi ubora na hatimaye iweze kuuzwa kwa bei nzuri”. Amesisitiza Katibu Tawala huyo.
Awali akizungumzia tukio hilo, Meneja wa Bodi ya Kahawa Mkoa wa Ruvuma Bw. Peter Buberwa amesema Maadhimisho ya Siku ya Kahawa Duniani hufanyika kila Oktoba Mosi ya kila mwaka na kwamba maadhimisho haya kwa mwaka huu yenye Kauli Mbiu isemayo ZALISHA KWA TIJA NA KUNYWA KAHAWA KWA AFYA yana lengo kuu la kuongeza hamasa ya unywaji wa kahawa nchini ambao upo chini kwa kiwango cha 7-10% ya uzalishaji na kuleta tija katika uzalishaji ambao bado upo chini kwa wastani wa robo kilo mpaka nusu kilo kwa mti wa kahawa.
Imeandikwa na
Salum Said, Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga
Oktoba 1, 2021
MBINGA DISTRICT COUNCIL
Sanduku la posta: P.O. BOX 194 MBINGA-RUVUMA
Namba za simu: 2552640005
SImu ya mkononi: PS 0754533018
parua pepe: ded@mbingadc.go.tz
Copyright ©2021 Mbinga District Council. All rights Reserved. Prepared by ICT - Unit