Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Mhe. Aziza Mangosongo ametoa wito kwa wazazi na walezi kutimiza majukumu yao ya msingi ndani ya familia ili kuimarisha hali ya upendo na kuepusha migogoro ya kila mara inayopelekea familia nyingi kusambaratika.
Akizungumza mbele ya wananchi waliojitokeza kwa wingi wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Familia Duniani Jumatatu Mei 15, 2023 yaliyofanyika viwanja vya Soko Kuu Mbinga Mjini, Mkuu huyo wa Wilaya amesema familia ni taasisi muhimu katika kujenga na kuimarisha jamii na taifa kwa ujumla lakini miaka ya hivi karibuni kumekuwepo wimbi la mmomonyoko wa maadili linalotokana na wazazi na walezi kutowajibika kikamilifu katika kutimiza majukumu yao ndani ya familia.
Aidha DC Mangosongo amekemea vitendo vya ukatili vinavyotokea kwenye familia huku akikumbushia umuhimu wa kuwa na maadili mema na kujenga dhana ya upendo miongoni mwa wanafamilia na jamii kwa ujumla.
"Nawaombeni tuendelee kuisaidia na kushirikiana na Serikali katika kuibua na kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia ndani ya familia na jamii zetu kwa kuhakikisha tunatoa taarifa za uwepo wa dalili na viashiria vyake kwenye mamlaka na vyombo vinavyohusika". Amesema DC Mangosongo.
Siku ya Kimataifa ya Familia Duniani huadhimishwa tarehe 15 ya kila mwaka huku mwaka huu 2023 yamefanyika katika maeneo mbalimbali nchini yakiwa na Kauli Mbiu isemayo Imarisha Maadili na Upendo kwa Familia Imara.
Akizungumzia maudhui ya maadhimisho haya Bi. Cecilia Mbata ambaye ni Afisa Maendeleo ya Jamii amesema ni katika kutambua umuhimu wa familia kama taasisi na chanzo cha jamii yoyote duniani na kwamba kauli mbiu ya mwaka huu inakumbusha umuhimu wa kuzingatia maadili mema katika malezi na makuzi ya watoto lakini pia inasisitiza suala la upendo miongoni mwa familia na jamii.
Imeandikwa na Salum Said,
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga
Tarehe 15 Mei, 2023
MBINGA DISTRICT COUNCIL
Sanduku la posta: P.O. BOX 194 MBINGA-RUVUMA
Namba za simu: 2552640005
SImu ya mkononi: PS 0754533018
parua pepe: ded@mbingadc.go.tz
Copyright ©2021 Mbinga District Council. All rights Reserved. Prepared by ICT - Unit