Wizara ya Maji kupitia Ofisi ya Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Nyasa imetoa saruji mifuko 150 na fedha tasilimu kiasi cha shilingi Laki Tano kwa wananchi na Jumuiya ya Watumia Maji Bonde Dogo la Mto Luwaita (JUWAMALU) ikiwa ni hatua ya kutambua na kuunga mkono jitihada zinazofanywa na wadau hao wa maji katika utunzaji na uhifadhi wa vyanzo vya maji kwenye maeneo mbalimbali ya Wilaya za Mbinga na Nyasa.
Hafla ya kukabidhi zawadi hizo kwa walengwa imefanyika leo Jumatatu tarehe 13 Machi 2023 katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Mgeni Rasmi akiwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas ambaye amekabidhi hati za unununuzi wa saruji mifuko 50 kwa kila Halmashauri kwa Wenyeviti watatu wa Halmashauri za Wilaya ya Mbinga, Halmashauri ya Mji Mbinga na Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa lakini pia akikabidhi risiti ya mapokezi ya fedha kwa mwenyekiti wa JUWAMALU.
Akitoa maelezo ya utangulizi kuhusiana na hafla hiyo Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Nyasa Mhandisi Elice Mnally amesema suala la zawadi ni utu lakini kutunza vyanzo vya maji ni wajibu wa kila mmoja na ni suala la maisha yetu, ustaarabu wetu na afya zetu kwa ujumla.
"Jitihada hizi tunazoziweka ni kwa sababu mkoa wa Ruvuma una vyanzo vingi vya maji na tuna wajibu wa kuhakikisha tunavitunza vyanzo hivi ili viweze kutusaidia kwenye maendeleo yetu ya kiuchumi lakini hata vizazi vinavyofuata." Amesisitiza Mhandisi Mnally na kuongeza kuwa utunzaji wa vyanzo vya maji linatakiwa kuwa kama desturi na wajibu wa kila mmoja.
Halfa hii imeandaliwa na Wizara ya Maji kupitia Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Nyasa na ni kufuatia ziara ya Waziri wa Maji Mhe. Juma Aweso mwaka 2022 alipotembelea miradi na vyanzo vya maji kwenye maeneo mbalimbali wilayani Mbinga na Nyasa na kuridhishwa na hali ya uhifadhi na utunzaji wa vyanzo hivyo ambapo alitoa ahadi ya kuchangia mifuko 150 ya saruji kwa ajili ya kuendeleza miradi ya maji ya jamii kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Halmashauri ya Mji Mbinga na Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa.
Imeandikwa na Salum Said
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga
MBINGA DISTRICT COUNCIL
Sanduku la posta: P.O. BOX 194 MBINGA-RUVUMA
Namba za simu: 2552640005
SImu ya mkononi: PS 0754533018
parua pepe: ded@mbingadc.go.tz
Copyright ©2021 Mbinga District Council. All rights Reserved. Prepared by ICT - Unit