Naibu Waziri wa Maji Mhe. MaryPrisca Mahundi leo Aprili 10, 2021 amefanya ziara ya kikazi Wilayani Mbinga ambapo ametembelea na kukagua mradi wa maji wa Kipapa na Mhilo ulitokelezwa kwenye Kata za Kipapa na Langiro, Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga wenye thamani ya shilingi Milioni 647.4 ambao umekamilika na umeanza kuhudumia wananchi kwa kutoa maji.
Katika ziara hiyo Mhe. Naibu Waziri ametoa mwezi mmoja kwa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mkoa wa Ruvuma wanaongeza vituo vya kuchotea maji kwenye kitongoji cha Kiosi, Kijiji cha Kipapa ndani ya mwezi mmoja ili kurahisisha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi wa eneo pamoja na kuhakikisha wanaanza utekelezaji wa mradi wa kusambaza maji kwenye Kijiji cha Langiro Asili, Kata ya Langiro ndani ya kipindi cha miezi mitatu ijayo.
Maagizo hayo ni kufuatia maombi ya wananchi kwenye maeneo hayo kwa Naibu Waziri wakati alipozungumza na kusikiliza malalamiko na kero zao; huku pia wananchi hao wakiishukuru Serikali kwa mradi huo muhimu na kwamba sasa wamerahisishiwa sana kwenye upatikanaji wa huduma hiyo muhimu ya maji.
Pamoja na mradi huo, pia Mhe. Naibu Waziri wa Maji ametembelea na kukagua miradi mingine miwili ya maji ambayo ni ule unaotekelezwa Kijiji cha Lifakara na unaokadiriwa kugharimu Shilingi Milioni 651 na mradi unaojengwa eneo la Kata ya Bethlehemu ambao unategemewa kugharimu Bilioni 1.4 hadi kukamilika kwake; yote hii ikitekelezwa Mbinga Mjini.
Kufuatia ziara hiyo Mhe. Naibu ametoa wito kwa wananchi kwenye maeneo yote ambayo miradi ya maji inatekelezwa nchini kuhakikisha wanatunza vyanzo vya maji sambamba na miundominu ya maji iliyopo kwenye maeneo yao ili miradi hiyo iweze kudumu kwa muda mrefu na kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
Mhe.Naibu Waziri wa Maji ataendelea na ziara yake kesho Aprili 11 Wilayani ambapo anatarajia kutembelea miradi ya maji inayotekelezwa kwenye vijiji vya Amani Makolo, Mabuni, Luhagara na Litumbandyosi, ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga.
Imeandikwa na
Salum Said,
Afisa Habari, Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga
MBINGA DISTRICT COUNCIL
Sanduku la posta: P.O. BOX 194 MBINGA-RUVUMA
Namba za simu: 2552640005
SImu ya mkononi: PS 0754533018
parua pepe: ded@mbingadc.go.tz
Copyright ©2021 Mbinga District Council. All rights Reserved. Prepared by ICT - Unit